Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukio la SDGs laadhimishwa kwa mara ya kwanza 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akifungua tukio la kwanza la Malengo ya maendeleo endelevu SDGs.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akifungua tukio la kwanza la Malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Tukio la SDGs laadhimishwa kwa mara ya kwanza 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo amefungua tukio la Malengo ya maendeleo endelevu, SDG jijini New York Marekani ambalo litakuwa linafanyika kila mwaka katika miaka hii kumi ya kuelekea kutimiza malengo hayo ifikapo mwaka 2030. Bwana Guterres ameuambia ulimwengu kupitia mkutano hio kuwa tukio hili la kujadili masuala ya malengo endelevu ni fursa kuonesha kuwa kama familia moja ya mataifa iliyoungana, “tuna kila kinachotakiwa ili kutokomeza umaskini na njaa, kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kufikia usawa wa kijinsia na kufanikisha malengo 17 ya kimataifa.”  

Akizungumzia COVID-19, Katibu Mkuu Guterres amesema janga hili la virusi vya corona linaharibu maisha na vyanzo vya kuendeshea maisha kote duniani na hivyo  uharaka wa kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu ni njia ya kufikia ulimwengu wenye afya, haki na amani zaidi.  

Tukio hili la kwanza la malengo ya maendeleo endelevu lililoitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, limewakutanisha kwa njia ya video, Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Malala Yousafzai ambaye pia ni mwanaharakati wa elimu na pia wawakilishi wa serikali mbalimbali, asasi za kiraia, mamlaka wenyeji, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi.  

 “Malengo ya maendeleo endelevu ni ajenda ya kumaliza umaskini na njaa, kudhibiti janga la mabadiliko ya tabianchi, kufikia usawa wa kijinsia na mengine zaidi katika miaka kumi ijayo.” Amesema Bwana Guterres.  

Aidha Bwana Guterres ameeleza kuwa tangu kupitishwa kwa malengo ya maendeleo endelevu kuna hatua ambazo zimepigwa kama vile afya ya mama na mtoto imekuwa ikiendelea kuwa bora, kupanua upatakianaji wa umeme na kuongeza uwakilishi wa wanawake.  

Tweet URL

 

Malala Yousafzai afunguka 

Naye Mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Malala Yousafzai amewapa changamoto nchi wanacahama akisema, Malengo ya maendeleo endelevu yanawakilisha mstakabali wa mamilioni ya wasichana ambao wanataka elimu, wanawake wanaopigania usawa, na vijana wanaopigania hewa safi, ni lini mnapanga kuifanya kazi?” 

Malala ameongeza kusema, “nilipoongea mara ya mwisho hapa, nilikuwa naelekea kuingia chuo kikuu…nikiwa na matumaini na kile kilichokuwa mbele: maisha ya chuoni, kupata marafiki wapya na kupata elimu bora. Mwezi wa June mwaka huu nilihitimu katikati ya ulimwengu wenye wasiwasi ambao wengi wetu wasingeweza kuutabiri.”  

Na ndipo Malala akawakumbusha viongozi kuwa miaka mitano iliyopita walitia Saini kwenye SDGs lakini, “hadi kufikia sasa hamjaendelea na kazi yenu. Ingawa COVID 19 imerudisha nyuma malengo yetu ya pamoja lakini haiwezi kuwa kisingizio. Katika elimu pekee, wasichana zaidi, milioni 20 wanawezawasirejee darasani wakati janga hili litakapoisha na pengo la ufadhili wa kimataifa kwa elimu tayari limeongezeka had idola bilioni 200 kwa mwaka.” 

SDGs zinatupa ramani 

Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 75 Volkan Bozkir, kwa upande wake pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa dunia inahitaji mshikamano, ushirika na mazungumzo. 

Volkan Bozkir, Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 75 akizungumza katika tukio la Malengo ya maendeleo endelevu SDGs.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Volkan Bozkir, Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 75 akizungumza katika tukio la Malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

 

“Kudhibiti kuasambaa kwa COVID-19 na kurudisha uendelezaji wa Malengo ya maendeleo endelevu, vinatakiwa kuwa vipaumbele vyetu vya pamoja.” Amesema Bwana Bozkir na kutaka kuwa nchi  hali fulani ya kipee kupewa kipaumbele.  

 “Haitakuwa rahisi lakini SDGs zenyewe zinatupatia ramani inayohitajika ili kupona, vizuri.” Amesisitiza Bwana Bozkir.