Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano katika kodi, fursa za kidijitali na udhibiti maliasili ni ufunguo wa kujikwamua baada ya COVID-19:UN

Jiji la Nairobi, Kenya
World Bank/Sambrian Mbaabu
Jiji la Nairobi, Kenya

Ushirikiano katika kodi, fursa za kidijitali na udhibiti maliasili ni ufunguo wa kujikwamua baada ya COVID-19:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wataalam ambao ni wajumbe wa Baraza la ushauri kwa ajili ya masuala ya kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa (DESA) leo wamechapisha ripoti inayopendekeza mambo ya kuzingatia kwa ajili ya kujikwamua vyema baada ya janga la corona au COVID-19 duniani.

Mapendekezo ya wataaalam hao yanalenga kushauri kuhusu ufikiaji wa malengo yote 17 ya maendeleo endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 huku wakitilia maanani tishio la milipuko ya majanga na athari zake katika ngazi ya kiuchumi na kijamii.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyowekwa kwenye ripoti na wataalam hao ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, kuhakikisha fursa sawa zaidi katika maendeleo ya teknolojia ya kidijitali, udhibiti endelevu wa maliasili lakini pia mitazamo yenye thamani katika biashara ya bidhaa.

Pia ripoti yao pia imeangazia hali ya sintofahamu inayoukabili uchumi wa dunia, kuweka mwenendo wa uchumi katika historia na kuelezea kwa nini mtazamo maalum wa maendeleo ya kiuchumi unahitajika.

Mapendekezo yao pia yametoa wito wa kuongeza msukomo katika masuala ya mazingira katika kusaka maendeleo ya kiuchumi na kijamii na msukomo zaidi uwekwe katika haja ya kuwa na ufadhili endelevu na usawa.

Akisisitiza hilo msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya kiuchumi na kijamii Liu Zhenmin amesema “Katikati ya janga la COVID-19 jumuiya ya kimataifa imejikuta katika hali isiyotarajiwa na isi yo ya kawaida. Vitisho vingine vinavyohusiana na afya, uchumi na migogoro ya kijamii vimedhoofisha nchi na kutuacha njiapanda. Watu masikini wa kutupa na wasiojiweza ndio walioathirika zaidi wakiwepo ia wanawake na watoto.”

Watu milioni 71 kutumbukia katika ufukara

Mapema mwezi huu ripoti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa ya ufuatiliaji wa maendeleo ya ufikiani wa malengo 17 ya SDGs imeonyesha kwamba ni watu masikini zaidi na walio hatarini ndio walioathirika vibaya na athari za COVID-19.

Na kukadiria kwamba takriban watu milioni 71 wanatarajiwa kutumbukia tena katika umasikini uliokithiri mwaka huu wa 2020 ikiwa ni ongezeko la kwanza la umasikini kimataifa tangu mwaka 1998.

Kwa upande wa maendeleo ya teknolojia ya kidijitali watalaam hao wametoa wito wa kuchagiza utafiti na maendeleo, kuwekeza katika miundombinu na elimu, kuanzisha kanuni za ufuatiliaji ili kuhakikisha mpangilio wa mikakati inayowekwenda sanjari na teknolojia inaongeza mishahara hususan kwa wafanyakazi wenye vipato vya chini na kuboresha usawa wa kiuchumi.

Changamoto za kidijitali zinaonyesha kiwango cha maamuzi magumu yanayowakabili wafanya maamuzi katika nia yao ya ukuaji endelevu na ajira zenye hadhi kupitia mabadiliko ya kimfumo. “Mada hii imekuja wakati muafaka na ni muhimu sana katika dunia baada ya COVID-19 ambayo itakuwa ni ya kidijitali zaidi yaha po kabla.” Ameongeza bwana Liu.

Lazima wote kuongeza juhudi

Mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ya ushauri ya Umoja wa Msataifa ni matokeo ya miaka miwili ya majadiliano na kazi kubwa iliyofanywa na wajumbe 17ambao wengi wao ni wanazuoni na watafiti wa masuala ya kiuchumi na pia wanasiasa wafanya maamuzi.

Miongoni mwa wajumbe hao ni mchumi wa Marekani kutoka chou kikuu cha Columbia Jeffrey Sachs ambaye amefanyaka kazi kwa miaka mingi kuhusu masuala ya maendeleo endelevu kwenye Umoja wa Mataifa na Joseph E. Stinglitz mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel katika masuala ya uchumi.

Wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya wajumbe hao Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amekumbusha kwamba malengo ya SDGs yanasalia kuwa ni mkakati wa makubaliano kwa ajili ya kujikwamua vyema baada ya COVID-19 ambao unachapuza mchakato wa vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, umasikini na pengo la usawa huku ukishughulikia hali ya kutokuwepo na usawa na hatari ambazo zimejitokeza au kuchangiwa na janga la corona.

Ameongeza kuwa “hakuna nchi ambayo itaendelea kama tutawaacha watu wengine nyuma. Ili kujikwamua vyema wote tunahitaji kuongeza juhudi zaidi.” amesisitiza Bi. Amina Mohammed.