Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yagawa redio 500 za sola kusaidia watoto kusoma wakati huu wa COVID-19

Mwanahabari wa Redio Miraya Sudan Kusini akizungumza na mtoto (Picha ya maktaba)
UNMISS/Isaac Billy
Mwanahabari wa Redio Miraya Sudan Kusini akizungumza na mtoto (Picha ya maktaba)

UNMISS yagawa redio 500 za sola kusaidia watoto kusoma wakati huu wa COVID-19

Utamaduni na Elimu

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umegawa redio 500 zinazotumia sola kwa jamii za Yambio , jimbo la Equatoria Magharibi ili kuwasaidia watoto waliosalia majumbani kutokana na janga la corona au COVID-19 kuweza kusoma.

Katika moja ya vijiji vya Yambio watoto wakiwa wamekusanyika nje pamoja wakisikiliza masomo kwa njia ya Redio ambazo zimesambazwa na UNMISS.

Redio hizo ambazo ni muhimu kwa wanafunzi kuhakikisha wanapata elimu wakati huu wa COVID-19 zimepatikana kwa msaada wa mradi wa kusomea majumbani ulioanzishwa na wizara ya elimu ya Sudan Kusini kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Sasa watoto hawa wanaweza kuhudhuria masomo kwa njia ya redio lakini pia kupata ujumbe wa kujikinga na COVID-19 unaotolewa kupitia matangazo ya Redio Miraya ya UNMISS

Msaada huu umekuja baada ya shule kufungwaSudan Kusini kwa karibu mezi minne sasa hali ambayo imewafanya watoto wengi kukosa masomo. Ipai Mary ni mmoja wa wanafunzi hao,"tunahitaji serikali na washirika wengine kutusaidia, wasichana wengi wanapata mimba kwa sababu shule zimefungwa. Tumekosa shule kwa miezi minne tukikaa nyumbani. Lakini sasa tunaishukuru UNMISS"

Viongozi wa jamii na wazazi  wa Yambio wameishukuru UNMISS kwa kugawa Redio hizo ambazo zinahakikisha jamii zinapata ujumbe kuhusu COVID-19 na watoto wanasoma. Yunnis Roma Danieli ni mmoja wa wazazi mjini Yambio,"kwa sababu ya corona shule zote zimefungwa na hakuna njia kwa watoto wetu kwenda madarasani. Redio hizi zitawasaidia wakati huu ambapo shule zimefungwa. Tumefurahi sana na tunaishukuru UNMISS kwa kuwapa watoto wetu redio hizi , pia tutapata taarifa kuhusu corona na jinsi ya kujikinga"

Na kwa UNMISS hilo ndilo lilikuwa lengo kuu kama anavyosema afisa wa ulinzi wa watoto wa mpango huo mjini Yambio Moses Bagari, "redio hizi zinatolewa kwa lengo maalum ili watoto wapate fursa ya kusoma kati ya saa 4 hadi saa 5 asubuhi na saa 9 hadi saa 11 jioni kila wiki. Pili ni kusaidia kikosi kazi cha serikali cha COVID-19 kuelimisha kuhusu njia za kujikinga dhidi ya corona."

Masomo hayo hutolewa kupitia Redio ya UNMISS ambayo ni Redio Miraya mara mbili kwa siku kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.