Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 9 kati ya 10 wanavuta hewa chafu, ni wakati wa kubadili hilo sasa:Guterres 

Ndege akiruka katika anga ya blu
UN News/Dina Neskorozhana
Ndege akiruka katika anga ya blu

Watu 9 kati ya 10 wanavuta hewa chafu, ni wakati wa kubadili hilo sasa:Guterres 

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema huu ni wakati wa kushikamana na kuchukua hatua zinazohitajika dhidi ya hewa chafu inayovutwa na watu 9 kati ya 10 kila uchao duniani kote.

Kupitia ujumbe wake wa maadhimisho ya kwanza kabisa ya siku ya kimataifa ya hewa safi kwa ajili ya anga ya blu, Guterres ameonya kwamba hewa chafu inayovutwa inachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani ya mapafu na magonjwa mengine ya mfumo wa hewa. 
Ameongeza kuwa “Inasababisha takriban vifo milioni 7 visivyo vya lazima kila mwaka hususan katika nchi za kipato cha chini na cha wastani. Uchafuzi wa hewa pia unatishia uchumi , uhakika wa chakula na mazingira.” 
 
Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu imesema wakati huu ambapo dunia inajikwamua kutoka kwenye janga la corona au COVID-19, dunia inapaswa kutoa msukumo mkubwa kuhusu suala la uchafuzi wa hewa ambao pia unaongeza hatari zinazohusiana na COVID-19. 
 
Amesisitiza kwamba “Ni lazima pia tushughulikie haraka tishio kubwa la mabadiliko ya tabianchi, kuhakikisha ongezeko la joto duniani linasalia nyuzi joto 1.5 hali ambayo itasaidia kupunguza uchafuzi wa hewa, vifo na magonjwa.” 
Picha inayoonyesha tofauti ya mji wa Beijing, uchaguzi wa hewa na anga ya blu
UN News
Picha inayoonyesha tofauti ya mji wa Beijing, uchaguzi wa hewa na anga ya blu
 
Akitoa mfano amesema mwaka huu hatua za kudhibiti kusambaa kwa corona zilizolazimisha kufungwa kila kitu na watu kusalia majumbani zimesaidia kiwango cha hewa chafuzi kushuka kwa kiasi kikubwa na hivyo kutoa matumaini ya hewa safi katika miji mingi. 
Hata hivyo ameonya kwamba uchafuzi wa hewa tayari unaongezeka tena na katika baadhi ya maeneo zaidi  hata ilivyokuwa kabla ya COVID-19, hivyo amesma “Kuliko wakati mwingine wowote sasa tunahitaji mabadilio makubwa na ya kimakati . Kusisitiza hatua za viwango vya mazingira, sera na sheria ambazo zinazuia wachafuzi wa hewa.” 
 
Guterres amezitaka nchi pia kuacha kutoa uzuku kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya kisukuku.Katika ngazi  kimataifa amezitaka nchi kushirikiana
ili kusaidiana kuingia katika teknolojia  za hewa safi. 
Ametoa wito kwa serikali mbazo bado zinafadhili miradi ya mafuta kisukuku katika chi zinazoendelea kuelekeza ufadhili huo kwenye nishati safi na usafiri endelevu. 
Pia amezitaka nchi zote kutumia fungu la kujikwamua baada ya COVID-19 kusaidia kuunga mkono mabadiliko ya kuingia katika ajira zenye afya na ndelevu. 
Siku  kimataifa ya hewa safi kwa ajili ya anga ya blu itaendelea kuadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Septemba kuanzia mwaka huu na katika maadhimisho haya ya kwanza kabisa Guterres ametaka ushirikiano kwa ajili ya kujenga mustakabali wenye hewa safi kwa wote.