Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kurejesha misitu kunaweza kusaidia ulimwengu kupona kutoka kwenye janga la corona.  

Njia ya kuelekea msituni
Unsplash/Lukasz Szmigiel
Njia ya kuelekea msituni

Kurejesha misitu kunaweza kusaidia ulimwengu kupona kutoka kwenye janga la corona.  

Tabianchi na mazingira

Juhudi za kupona kutoka kwenye janga lililosababishwa na COVID-19 zinapaswa kusababisha hatua kali ya kuokoa misitu ya ulimwengu, amesema Liu Zhenmin, msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya kiuchumi na kijamii pia akisisitiza ni kiasi gani maliasili hizi zimesaidia kulinda afya na ustawi wakati wa janga hili ulimwengu. 

"Pamoja na umuhimu wake dhahiri, misitu inaendelea kutishiwa." Amesema Liu na kuongeza, “kila mwaka, hekta milioni saba za misitu ya asili hubadilishwa kuwa matumizi mengine ya ardhi, kama kilimo kikubwa cha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi. Na wakati kiwango cha ukataji miti kimepungua katika muongo mmoja uliopita, upotezaji wa miti umeendelea bila kukoma kutokana na sababu za kibinadamu na asili.” 

Liu Zhenmin ametoa wito huo katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Misitu, ambayo huadhimishwa kila mwaka mwezi Machi 21. 

Aidha amesema sekta ya misitu ilitoa bidhaa muhimu na za kuokoa maisha wakati wa janga la corona, kama vile vinyago, bidhaa za kusafisha na ethanoli inayotumiwa katika dawa za kuua wadudu. 

Umoja wa Mataifa unaamini kuwa usimamizi endelevu wa misitu ni muhimu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha maisha bora ya baadaye. 

Kaulimbiu ya ya mwaka huu ni "Urejeshaji wa Misitu: sauti ya kupona na ustawi" pia inaendana na Muongo wa Umoja wa Mataifa wa kurejeshwa kwa Ekolojia, 2021 hadi 2030.