Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitendo vya uharibifu wa mazingira vyasababisha mazingira kutuma ujumbe - Guterres 

Kimbuga Idai kilichopita mji wa Beira nchini Msumbiji mwaka 2019 kilikuwa na madhara makubwa.Pichani wananchi wakiendelea kupokea msaada mwaka mmoja tangu janga hilo.
ICRC/Anette Selmer-Andresen
Kimbuga Idai kilichopita mji wa Beira nchini Msumbiji mwaka 2019 kilikuwa na madhara makubwa.Pichani wananchi wakiendelea kupokea msaada mwaka mmoja tangu janga hilo.

Vitendo vya uharibifu wa mazingira vyasababisha mazingira kutuma ujumbe - Guterres 

Tabianchi na mazingira

Mazingira yanatutumia ujumbe dhahiri ya kwamba tunaharibu mazingira yetu ya asili kwa hasa yetu wenyewe,  hivyo ndiyo alivyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya mazingira duniani hii leo Juni 5, maudhui yakiwa bayonuai.

Katibu Mkuu anasema kuwa uharibifu wa mazingira na bayonuai unafanyika kwa kasi kubwa huku tabianchi nayo inazidi kusambaratika kila uchao.

Anasema kuwa, “mioto, mafuriko, ukame na vimbunga vikubwa kupita kiasi vinatokea mara kwa mara hivi sasa na vinasababisha uharibifu. Kiwango cha joto na aside baharini kinaongezeka huku vikiharibu mifumo anuai ya matumbawe. Na sasa virusi vipya vya Corona vinaharibu afya na mbinu za kipato.”

Guterres anasema kuwa, kutunza ubinadamu ni lazima kutunza mazingira na “tunahitaji jamii nzima ya kimataifa kubadili mwelekeo. Hebu tufikirie upya kile tununuacho na  tutumiavyo.”

 Na zaidi ya yote Katibu Mkuu anasema kuwa, ‘tufuate mbinu endelevu kitabia, kwenye kilimo na kwenye biashara Tulinde maeneo yaliyosalia ya wanyaporo na tuahidi mustakabali usioharibu mazingira na wenye mnepo.”

Askari wa zimamoto huko Queensland, Australia wakikabiliana na moto uliotishia makazi ya jamii.
Queensland Fire and Emergency Services
Askari wa zimamoto huko Queensland, Australia wakikabiliana na moto uliotishia makazi ya jamii.

 Bwana Guterres anasema kuwa wakati huu jamii ya kimataifa inafanya kazi kurejesha hali bora, “hebu na turejeshe mazingira katika hali yake, katika kitovu cha hatua zetu za kupitisha maamuzi. Na katika siku ya mazingira duniani hii leo ni wakati wa mazingira.”

 Siku ya mazingira duniani ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 15  mwezi Desemba mwaka 1972 kupitia azimio namba A/2994 (XXVII).

Mwaka huu maadhimisho yanafanyika kukiwa na matukio ya kutia hofu kama vile mioto ya nyika nchini Brazil, Marekani na Australia na baa la nzige Mashariki mwa Afrika na sasa janga la COVID-19, hali ambao Umoja wa Mataifa inasema kuwa inaonesha uhusiano mkubwa kati ya binadamu na mazingira.

UNEP yataka kupima uelewa wako kuhusu bayonuai

Je wafahamu nini kuhusu bayonuai na uhusiano wake na mazingira na mle ambamo binadamu na wanyama wanaishi? Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP linakukaribisha ufanye zoezi lifuatalo upime uelewa wako.