Mto Nile umejaa pomoni na kusababisha mafuriko makubwa Sudan:OCHA 

1 Septemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA limesema mvua kubwa zinazonyesha hususan nchini Ethiopia zimesababisha mafuriko makubwa nchini Sudan baada ya mwisho wa wiki mto Nile kujaa pomoni, maji yakifikia karibu mita 17.5 kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 100. 

Mjini Khartoum pekee kwa mujibu wa serikali ya Sudan na OCHA  zaidi ya watu 21,000 wameathirika na mafuriko hayo tangu mwisho wa mwezi wa Julai na Jumapili serikali ilitangaza hali ya dharura katika jimbo hilo. 

Akizungumza na waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao hii leo mjini Geneva Uswisi msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema “Katika nchi nzima kufikia tarehe 25 Agosti watu 380,000 wamearifiwa kuathirika na mafuriko hayo na 90 wameuawa. Nyumba 37,000 zimebomolewa na kuzilazimisha familia kusaka hifadhi kwa ndungu na jamii. Nyumba zingine 39,000 zimeharibiwa vibaya ikiwa ni Pamoja na shule 34 na karibu vituo vya afya 2,700.” 

Hatari ya kukosa maji wakati wa COVID-19 

Ameongeza kuwa fursa ya kupata maji safi na salama ambayo ni muhimu wakati huu wa janga la corona au COVID-19 pia imeathirika. Takriban vyanzo vya maji 2000 vimechafuliwa au havifanyi kazi kutokana na tathimini ya awali.  

OCHA imesema wakati mji wa Khartoum sasa uko katika hali ya dharura mahitaji ya haraka ni kuziba kingo za mto Nile na kutoa huduma ya malazi kwa wasio na pakuishi. 

Kwingineko nchi nzima Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wansaidia hatua za kitaifa kwa msaada wa dharura wa malazi na vifaa vya nyumbani, maji, usafi na vifaa vya kujisafi, chakula, huduma za afya na kudhibiti wadudu. 

Maandalizi yamesaidia 

Shirika hilo la kibinadamu la Umoja wa Mataifa limesema hatua za haraka zimewezekana kwa sababu serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau walijipanga mapema na kuandaa misaada ili kuchukua hatua kukidhi mahitaji ya watu 250,000 hata kabla mvua hazijaanza. 

Hata hivyo shirika hilo limeongeza kwamba akiba hiyo inakwisha haraka.”Hivyo tunatoa wito wa msaada zaidi kutoka kwa wahisani ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watu walioathirika na mafuriko na kuweza kuendelea na msaada wetu wa kawaida wa kibinadamu nchi nzima.” 

Mpango wa msaada wa kibinadamu kwa ajili ya Sudan mwaka 2020 (HRP) ambao ulitoa ombi la dola bilioni 1.6 umefadhiliwa chini ya asilimia 44 hadi sasa. 

  

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud