Watu 100 wapoteza maisha na zaidi ya laki 5 waathirika na mafuriko Sudan:OCHA 

8 Septemba 2020

Watu 100 wamepoteza maisha na zaidi ya laki 5 wameathirika na mafuriko makubwa yanayoendelea nchini Sudan ambayo yalianza katikati ya mwezi Julai na sasa wanahitaji haraka msaada wa huduma za msingi , limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA. 

OCHA inasema mafuriko hayo yameshika kasi wiki iliyopita na kusababisha mafuriko makubwa, watu kutawanywa na wengine kupoteza maisha . Tarehe 4 mwezi huu wa Septemba serikali ya Sudan imetangaza miezi mitatu ya hali ya dharura nchi nzima kufuatia mafuriko hayo. 

Kwa mujibu wa OCHA jumla ya watu 506,000 wameathirika na wengine110,000 miongoni mwao katika wiki ya kwanza tu ya mwezi huu wa Septemba.  

Picha za sateliti zinaonyesha mafuriko hayo pia yameharibu zaidi ya kilometa 500 za ardhi mjini Khartoum, Al Geriza na jimbo la White Nile na karibu watu 100 wamekufa kutokana na mafuriko hayo na maporomoko ya udongo, ambayo pia yamejeruhi watu wengine 46.

Maelfu ya watu waliotawanywa wengi wao wamesaka makazi ya muda kwenye shule mbalimbali wakati huu ambao shule zinatarajiwa kufunguliwa. 

OCHA inasema serikali ya Sudan, mashirika ya Umoja wa Mataifa na sekta binafsi wanatoa msaada wa kuokoa maisha kwa maelfu ya watu kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo, hata hivyo idadi ya waathirika imezidi makadirio ya awali ya watu 250,000 na mashirika hayo yanapungukiwa msaada hasa vifaa vya malazi, vifaa visivyo chakula kama vyombo vya jikoni, madumu ya maji, maturubahi, vifaa tiba, maji na vifaa vya kujisafi na usafi. 

OCHA imeonya kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo kwani mvua inatarajiwa kuongezeka nchini Ethiopia na katika sehemu nyingi za Sudan na hivyo kuongeza kina cha maji kwenye mto Blue Nile na kusababisha mafuriko zaidi. 

Shirika hilo limetoa wito wa msaada wa haraka kutoka kwa wahisani na jumuiya ya kimataifa ili kuongeza akiba ya misaada na kuendelea kuwahudumia wahitaji. 

Ombi la msaada wa dola bilioni 1.6 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu Sudan lililotolewa mwaka huu wa 2020 hadi sasa ni asilimia 44 u a feda ndio zimeshapatikana. 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter