Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 ni tishio kwa maendeleo endelevu:Guterres

Nchini India, wanawake wakionesha jinsi ya kutumia ungo wa nishati ya jua kwa ajili ya kupikia.
UNDP India
Nchini India, wanawake wakionesha jinsi ya kutumia ungo wa nishati ya jua kwa ajili ya kupikia.

COVID-19 ni tishio kwa maendeleo endelevu:Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la corona au COVID-19 limeanika wazi mifumo tete na pengo la usawa vitu ambavyo vinatishia msingi wa maendeleo endelevu, SDGs. 

 

Katika hotuba yake leo kwa ajili ya kumbukumbu ya 19 ya Darbari Seth nchini india iliyopewa jina “kuibuka kwa nishati jadidifu, kunatoa mwangaza kuhusu mustakbali endelevu” Katibu Mkuu amesema ongezeko la joto duniani linatishia hata zaidi kuvuruga na kuweka bayana athari za pengo kubwa lililopo duniani. 

Ameongeza kuwa Wakati tukitarajia kujikwamua kutoka kwenye janga la COVID-19, lazima tuahidi kufanya vyema zaidi ya sasa. Hii inamaanisha kufanyia mabadiliko uchumi wetu, nishati na mifumo ya afya ili kuokoa maisha, kujenga mnepo, kuwa na uchumi jumuishi na kutokomeza tishio la mabadiliko ya tabianchi.” 

Kutokomeza umasikini na nishati safi ndio jibu 

Guterres amesema vichocheo vikubwa vya kufikia malengo hayo ni kutokomeza umasikini na fursa ya nishati kwa wote vitu viwili ambayo ni vipaumbele vya India.  

Kusongesha mbele matumizi ya nishati safi hususani sola ni chachu ya kutatua matatizo yote. 

Guterres amesisitiza kwamba “Uwekezaji katika nishati jadidifu , usafiri usiochafua mazingira na nishati toshelezi wakati wa kujikwamua na janga la corona kutaongeza fursa za upatikanaji umeme kwa watu milioni 270 kote duniani ikiwa ni theluthi ya idadi ya watu ambao sasa wanakosa nishati hiyo.” 

Ameongeza kuwa uwekezaji huohuo utasaidia kuunda ajira milioni 9 kila mwaka katika miaka mitatu ijayo. Kwani uwekezaji katika nishati jadidifu unaongeza ajira mara tatu zaidi kuliko uwekezaji katika nishati zinazoharibu mazingira. 

Pamoja na jitihada India bado ina changamoto 

Antonio Guterres amesema wakati janga la COVID-19 linatishia kuwatumbukiza tena mamilioni ya watu katika umasikini, India imepiga hatua kubwa kuelekea fursa ya nishati ya umeme kwa wote. 

Lakini licha ya fursa ya hiyo ya kiwango cha asilimia 94, watu milioni 64 nchini India leo hii bado hawana  nishati hiyo na ruzuku ya nishati zinazochafua mazingira ni mara saba zaidi ya ruzuku ya nishati safi. "Kuendelea kuunga mkono nishati chafuzi katika sehemu mbalimbali kote duniani ni suala linalosumbua sana. Nimeziomba nchi zote 20 tajiri ikiwemo india kuwekeza katika nishati safi na inayojali mazingirawakati zikiendelea kujikwamua kutoka kwenye janga la COVID-19. Hii inamaanisha kukomesha ruzuku kwa nishati chafuzi, kuongeza gharama kwa uchafuzi wa hewa ukaa na kuahidi kutozalisha mitambo mipya ya makaa yam awe baada ya 2020.”

Mienendo inayotia mashaka 

Katibu Mkuu amesema anatiwa hofu kubwa na mienendo mibaya inayoongezeka. “Katika baadhi ya nchi tunashuhudia ongezeko mara mbili la matumizi ya makaa ya mawe na kufungua minada ya makaa hayo. Mkakati huu utachangia zaidi udorororaji wa uchumi na athari mbaya za afya. Endapo uchfuzi utokanao na makaa ya mawe utatokomezwa kwa ujumla umri wa kuishi kwa binadamu utaongezeka kwa miezi zaidi ya 20 na kuepuka vifo milioni 5.5 kwa mwaka.” 

Amesisitiza kwamba kuwekeza katika nishati hiyo inayochafua mazingira ni “janga la kibinadamu na pigo kwa uchumi.Na hii ni kwa sababu kwamba nishati jadidifu ni rahisi kuizalisha na kuijengea uwezo kuliko kuendesha asilimia 39 ya uwezo wa makaa ya mawe uliopo kote duniani.” 

 Amesema na hii ndio sababu wawekezaji wakubwa duniani wanaitelekeza sekta ya makaa ya mawe.  Wanaona maandishi yaliyoandikwa ukutani yasemayo mali iliyotelekezwa na isiyo na maana yoyote  kibiashara. Hivyo biashara ya makaa ya mawe inateketea. 

Mambo sita ya kuzingatia 

Katibu Mkuu katika hotuba hiyo amesema wakati serikali zikichangisha matrilioni ya dola ili kujikwamua na janga la COVID-19, maamuzi yao yatakuwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa miongo kadhaa ijayo. 

Hii ndio sababu amezitaka serikali kuchukua hatua sita chanya za mabadiliko ya tabianchi ili kujikwamua vyema kwenye janga hili ambazo ni  

  • Kuwekeza katika ajira zinazojali mazingira 
  • Kutoziwekea dhamana sekta zinazochafua mazingira 
  • Kukomesha ruzuku kwa ajili ya nishati chafuzi 
  • Kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi katika maamuzi ya fedha na sera 
  • Kufanya kazi kwa pamoja  
  • Na la msingi zaidi kutomwacha yeyote nyuma.