Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna nishati safi na fedha katika kinachoonekana kuwa ni takataka – FAO

Sukhdev Vishwakarma na binti yake Meenu wote wakiwa ni wakulima wanatu,mia maji ya kisima cha kupampu na sola katika shamba la Gurinder Singh lenye ukubwa wa ekari 80 Jagadhri.
© CCAFS/Prashanth Vishwanathan
Sukhdev Vishwakarma na binti yake Meenu wote wakiwa ni wakulima wanatu,mia maji ya kisima cha kupampu na sola katika shamba la Gurinder Singh lenye ukubwa wa ekari 80 Jagadhri.

Kuna nishati safi na fedha katika kinachoonekana kuwa ni takataka – FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kilimo ni moja ya shughuli za kibinadamu zinazochangia katika uchafuzi wa hewa. Kwa kulitambua hilo, FAO kote ulimwenguni inachagiza kile inachokiita kwa lugha ya kiingereza Bioeconomy yaani uchumi ambao msingi wake unatokana na matumizi ya rasilimali za kibayolojia zinazopatikana kwenye mazingira; kwa mfano kurejesha taka katika uzalishaji wa nishati safi, mbadala wa mafuta ya kisukuku. Kupitia harakati hizo, FAO inasaidia wakulima kuongeza mapato, kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kuchangia kupunguza taka ulimwenguni kwa kubadilisha mifumo ya zamani ya kilimo ambayo ilikuwa inachangia kuharibu mazingira.

 

FAO iliwatembelea wakulima wa mpunga katika eneo moja nchini India. Kama walivyo wakulima wengine katika maeneo mengine duniani, hawa nao walikuwa wanachoma moto mabaki ya mimea baada ya mavuno ili kuandaa shamba kwa ajili ya msimu mwingine. 

Njia hiyo isiyofaa ilimaanisha kuwa wakulima hawakufaidika na mabaki ya mimea ya mpunga lakini sasa wakulima na kampuni za biashara wanavuna pia kutoka katika mabaki hayo kwa kuzalisha nishati mbadala ya mafuta ya kuendeshea mitambo na pia vumbi la mabaki linatumika kutengeneza nishati, mbadala wa mkaa wa miti.

Profesa Ramesh Chand ambaye ni mmoja wa jopo la fikra la Serikali ya India linalohusika na sera za umma za kuchochea maendeleo ya kiuchumi, anasema, “kwa kuchoma moto tu mabaki ya mazao bila kuyatafutia shughuli mbadala sio tu unaharibu mazingira na afya bali pia kwa namna fulani unachoma moto utajiri.”