Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala wa aina yake wa ngazi ya juu kuhusu nishati unaofanyika Ijumaa hii, haujapata kutokea kwa takribani miaka 40  

Paneli za nishati ya jua zikitumika nchini Cambodia ili kufikia hitaji la nishati la nchi hiyo.
UNDP/Manuth Buth
Paneli za nishati ya jua zikitumika nchini Cambodia ili kufikia hitaji la nishati la nchi hiyo.

Mjadala wa aina yake wa ngazi ya juu kuhusu nishati unaofanyika Ijumaa hii, haujapata kutokea kwa takribani miaka 40  

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Sambamba na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 74/225, Katibu Mkuu Ijumaa hii ya tarehe 24 Septemba ameandaa mjadala wa ngazi ya juu wa Nishati wakati huu wa Mjadala Mkuu wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 ili kuharakisha utekelezaji wa lengo namba 7 la maendeleo endelevu linalohusiana na nishati endelevu.  

“Tunahitaji kuhakikisha nishati endelevu kwa wote kufikia mwaka 2030. Hili ni kusudio la lengo namba 7 la maendeleo enelevu, SDGs. Hivi sasa tunapungukiwa. Kwa sababu hiyo ninaitisha mkutano mwezi Septemba jijini New York.” Alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa miezi kadhaa iliyopita alipofanya maamuzi ya kuitisha mjadala huu. 

Ukiwa ni mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu nishati chini ya usimamizi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tangu Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Vyanzo vipya na jadidifu vya Nishati uliofanyika Nairobi mnamo mwaka 1981, mjadala wa sasa utawaleta pamoja wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia, mamlaka mitaa, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi pamoja na wadau wengine  kwa nia ya kuleta mabadiliko katika miaka ya kwanza ya Muongo Utekelezaji wa SDGs, Muongo wa Nishati Endelevu na kwa Wote na utekelezaji wa Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. 

Matokeo makuu ya Mjadala yatakuwa muhtasari ambao haujadiliwa wa Mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ikijumuisha ramani ya kuelekea mafanikio ya lengo namba 7 la maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 na uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi ifikapo mwalka 2050 na pia mfululizo wa "Mikataba ya Nishati ”, Kutoka kwa Nchi Wanachama na watendaji wasio wa serikali kama vile kampuni, miji na asasi za kiraia, wakionesha vitendo vyao vya uongozi na kujitolea kwa hiari kuelekea SDG7 na uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi.  

Mjadala huu umeandaliwa kiujumuishi kwani Nchi 30 wanachama waliongoza uhamasisha wa kimataifa na uhamasishaji wa Mikataba ya Nishati. Vikundi vitano vya wadau wa kiufundi, vinavyoongozwa pamoja na mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa na mengine ya kimataifa na kuungwa mkono na wataalam 160, walitoa ripoti tano kuarifu Mabaraza ya Mawaziri yaliyofanyika mnamo mwezi Juni mwaka huu wa 2021, kwa kuwakutanisha Mawaziri 50, wasemaji wataalam 330 na washiriki 1,500 na matukio 80 ya kandoni. Majadiliano wakati wa Mabaraza ya Mawaziri yaligundua vitu muhimu vya njia ya  ulimwengu kuelekea kufanikiwa kwa SDG namba 7 ifikapo mwaka 2030 na uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050. 

Nishati mbadala

Nishati zinazolengwa ni zile ambazo hazisababishi madhara kwa ulimwengu. Dunia inalenga kuacahana na matumizi ya mafuta kama vile ya kisukuku, makaa ya mawe, miti na mengine ya namna hiyo na kuhamia katika nishati jadidifu na pia endelevu kama matumizi ya nishati ya jua. 

Mtandaoni 

Mjadala huu wa ngazi ya juu unaofanyika Ijumaa hii pamoja na matukio mengine ya awali kandoni mwa mjadala huu yanafanyika kwa njia ya mtandao pekee. 

Washiriki 

Mjadala utakuwa wa wazi kwa Nchi Wanachama wote na wadau wengine. Washiriki wote wataweza kufuatilia mazungumzo kupitia matangazo ya moja kwa moja katika wa wavuti wa Mjadala wa ngazi za juu na pia katika UN Web TV Ijumaa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 12 jioni kwa saa za Marekani.