Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 172 zajiunga na COVAX mkakati wa kimataifa wa chanjo dhidi ya COVID-19: WHO

Huko Venezuela na kote ulimwenguni, utumiaji wa barakoa utabaki kama njia muhimu ya kujizuia dhidi ya  COVID-19, angalau hadi chanjo itakapopatikana.
© OCHA/Gema Cortes
Huko Venezuela na kote ulimwenguni, utumiaji wa barakoa utabaki kama njia muhimu ya kujizuia dhidi ya COVID-19, angalau hadi chanjo itakapopatikana.

Nchi 172 zajiunga na COVAX mkakati wa kimataifa wa chanjo dhidi ya COVID-19: WHO

Afya

Nchi 172 sasa zinashiriki katika mpango wa kimataifa wa fursa za siku za usoni kwa ajili ya upatikanaji wa chanjo dhidi ya janga la corona au COVID-19 ujulikanao kama COVAX, ambao umeundwa ili kuhakikisha fursa sawa za chanjo ya corona, limetangaza leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO.  

Akitoa tangazo hilo katika mkutano wa waandishi wa Habari kwa njia ya mtandao mjini Geneva Uswis , mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros AdhanomGhebreyesus amesema “Nina furaha kubwa kuripoti kwamba hadi kufikia leo nchi 172 zinashiriki katika mpango wa kimataifa wa huduma ya chanjo COVAX, ambao una mchanganyiko na asilimia kubwa kazaidi ya orodha ya chanjo za COVID-19 duniani.” 

Mpango wa COVAX unaongozwa na muungano wa chanjo duniani GAVI, WHO na muungano kwa ajili ya ubunifu wa kujiandaa na magonjwa ya mlipuko (CEPI). 

Na umeundwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba kuna fursa sawa za upatikanaji wa chanjo ambayo itatengenezwa na kuruhusiwa kutumika duniani. Hivi sasa ina aina 9 za chanjo za kupambana na COVID-19 ambazo zinauwezekano wa kutumiwa na lengo la COVAX ni kuhakikisha usambazaji na ufikishaji wa dozi bilioni 2 kwa nchi ambazo zitajiunga ifikapo mwisho wa mwaka 2021. 

Dkt. Tedros katika tangazo lake ameongeza kuwa “Hivi sasa chanjo 9 ni sehemu ya orodha hiyo ambayo inafanyiwa tathimini kila wakati na kuhakikiwa ili kuhakikisha fursa ya uwezekano wa kuwa na dawa bora zaidi. Majadiliano tayari yanaendelea na wazalishaji wengine wane. Chanjo zingine 9 hivi sasa zinachunguzwa kwa ajili ya mipango ya muda mrefu.” 

Angalau dozi bilioni 2 za chanjo mwisho wa 2021 

WHO inasema wakati usambazaji ukiongezeka , hatua inayofuata ya utoaji wa chanjo wigo wake utapanuliwa kwa misingi ya tathimini ya hatari ya kila kimchi ya virusi hivyo. 

Idadi kadaa ya chanjo kwa sasa ziko katika hatua za mwisho za majaribio. Na WHO inatumai kwamba kutakuwa na kadhaa mbazo zitafanikiwa kwenye mchakto na ambazo zitakuwa salama na zitakazofanya kazi. 

COVAX ni mkakati muhimu ambao utaruhusu nachi zote washiriki kuwa na fursa na chanjo hizo ambazo usalama na ufanyaji wake kazi umethibitishwa. 

Muuguzi akiwa amevalia barakoa anampatia huduma ya kwanza mtoto mchanga aliyezaliwa kwenye kituo cha afya cha Port Bouet, kilichoko katika viunga vya mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.
© UNICEF/UNI312809// Frank Dejongh
Muuguzi akiwa amevalia barakoa anampatia huduma ya kwanza mtoto mchanga aliyezaliwa kwenye kituo cha afya cha Port Bouet, kilichoko katika viunga vya mji wa Abidjan nchini Côte d'Ivoire.

Ameoneza kuwa wakati huohuo nchi zinazotaka kushiriki katika mpango huu wa kimataifa wa COVAX zinapewa hadi tarehe 31 Agosti kuwasilisha nia zao. 

Na thibitsho la nia zao za kujiunga ni lazima lifanywe ifikapo 18 Septemba na malipo ya awali kufanya ifikapo Oktoba 9. 

Kwa mujibu wa WHO COVAX ni kifaa maalum na cha muhimu kwa ajili ya ununuzi wa Pamoja na kufuatilia hatari zinazohusiana na chanjo mbalimbali ili kwamba chanjo yoyo te ambayo usalama na utendaji wake utakuwa umeidhinishwa nchi zote wanachama wa COVAX watakuwa na fursa nazo. 

Bwana. Tedros amesisitiza kwamba “La muhimu zaidi huu ni makakti ambao utaruhusu uratibu wa kimataifa wa usambazaji wake katika kiwango cha kimataifa. Ni katika maslahi ya nchi zote hata zile ambazo zimewekeza kwa wazalishaji binafsi peke yao.” 

Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19
UN Photo/Loey Felipe
Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19

Kwa mantiki hiyo WHO imekumbusha kwamba inashirikiana na wazalishaji wa chanjo ili kuzitaka nchi zote kuingia katika juhudi za Pamoja kuhakikisha fursa za haraka na sawa za upatikanaji wa chanjo ambazo zimedhibitishwa na kuidhinishwa. 

Tedros amesema “COVAX sio tu kwamba itadhibiti athari kwa nchi ambazo zinatengeneza na kuuza chanjo, lakini pia inamaanisha kwamba gharama itasalia chini iwezekanavyo.” 

Ameongeza kuwa ili kupata dozi za kutosha kwa utekelezaji wa chanjo hatua inayofuata katika ushirikiano huo ni kwa nchi kuweka ahadi zitakazowafunga za kusaidia mchakato wa COVAX. 

“Wakati tunashukuru kwa ufadhili wa fedha ambazo tayari zimeshaingizwa kwa COVAX, kuna haja ya haraka ya kuongeza juhudi kuendelea kusongesha mbele orodha yetu. Lengo la mchakato wa COVAX ni kufikisha angalau dozi bilioni 2 za chanjo zilizo salama na zinazofanya kazi ifikapo mwisho wa 2021.” 

Zaidi ya watu 800,000 wamepoteza maisha 

WHO inasisitiza kwamba mchakato huu utaleta mafanikio makubwa katika uwekezaji hasa wakati nchi zinawekeza mabilioni ya dola katika kujikwamua kiuchumi. 

“Kuna mwanga unaoonekana mwisho wa sakata hili na kama nilivyosema wiki iliyopita tunaweza kulifanikisha kwa pamoja. Wakati tukiwekeza kwa pamoja katika utafiti wa chanjo na maendeleo lazima pia tutumie nyenzo tulizonazo kwa sasa kutokomeza virusi hivi.” 

WHO inaamini kwamba uwekezaj ni njia ya haraka ya kumaliza janga la COVID-19 na kuhakikisha kujikwamua ambako ni endelevu kwa kiuchumi. 

COVAX itahakikisha kwamba nchi zote ziwe za kipato cha chini, kati na Tajiri zinapata chanjo kwa wakati mara tu chanjo ambayo itathibitishwa kuwa salama na inayofanyakazi itakapopatikana. 

Kwa mujibu wa takwimu za WHO idadi ya wagonjwa wa corona na vifo inaendelea kuongezeka kote duniani. Hadi sasa julma ya watu 805,902 wamepoteza Maisha miongoni mwa watu milioni 23.2 ambao wamethibitishwa kuwa na COVID-19.