Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya COVAXIN ya India ruksa kuitumia dhidi ya COVID-19:WHO

India imeanza mpango mkubwa zaidi duniani wa chanjo ya COVID-19.( Maktaba)
© UNICEF/Ruhani Kaur
India imeanza mpango mkubwa zaidi duniani wa chanjo ya COVID-19.( Maktaba)

Chanjo ya COVAXIN ya India ruksa kuitumia dhidi ya COVID-19:WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani (WHO)  leo limeidhinisha chanjo ya nane dhidi ya COVID-19, wakati huu kukiwa na ongezeko kidogo la wagonjwa wapya kote duniani.

Chanjo hiyo COVAXIN, iliyotengenezwa na kampuni ya India ya Bharat Biotech, kuidhinishwa kwa matumizi ya dharura na WHO (EUL), inamaanisha kwamba inaweza kupatikana kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote hivi karibuni.

Mchakato wa uidhinishaji wa matumizi ya dharura (EUL) hutathmini ubora, usalama na ufanisi wa chanjo na ni sharti la kujumuishwa kwao katika mpango wa kimataifa wa mshikamano wa upatikanaji wa chanjo, COVAX.

Kuendelea kuweka shinikizo

Pia idhini hiyo inaruhusu nchi kuharakisha uidhinishaji wao wa udhibiti wa kuagiza na kusimamia dozi za chanjo.

"Orodha hii ya matumizi ya dharura inapanua wigo wa upatikanaji wa chanjo na zana bora zaidi za matibabu tunazohitaji kumaliza janga hili," amesema Dkt. Mariângela Simão, mkurugenzi mkuu msaidizi wa WHO kwa kwa ajili ya upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya.

Ameongeza kuwa "Lakini lazima tuendeleze shinikizo ili kukidhi mahitaji ya watu wote, tukitoa kipaumbele kwa makundi yalivyo hatarini zaidi ambayo bado yanangojea dozi yao ya kwanza ya chanjo, kabla ya kuanza kutangaza ushindi."

COVAXIN ilikuwa tayari imeanza kutolewa nchini India, ambapo mamlaka ilikuwa imeidhinisha matumizi yake tangu Januari mwaka huu, ingawa awamu ya tatu ya majaribio ya kitibabu bado ilikuwa ikiendelea, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. Bharat Biotech baadaye ilitoa takwimu zinazoonyesha kuwa chanjo hiyo ilikuwa na ufanisi wa karibu asilimia 78.

Kukidhi viwango vya WHO

Kundi la washauri la WHO lilitathmini chanjo ya COVAXIN chini ya utaratibu wa EUL, kulingana na ukaguzi wa takwimu kuhusu ubora, usalama, ufanisi, mpango wa kudhibiti hatari na program ya upatikanaji wake.

Imeamriwa kuwa chanjo hiyo inakidhi viwango vya WHO vya ulinzi dhidi ya COVID-19, na kupewa ruksa ya kusambazwa ulimwenguni kote.

Mwezi uliopita, COVAXIN pia ilitathiminiwa upya na kundi la wataalamu wa ushauri wa mkakati wa chanjo wa WHO (SAGE), ambalo linaunda sera mahususi kuhusu chanjo na mapendekezo ya matumizi yake.
SAGE imependekeza matumizi ya COVAXIN kutolewa dozi mbili, kwa muda wa wiki nne, katika makundi yote ya watu wa umri wa zaidi ya miaka 18.

Mahitaji rahisi ya kuihifadhi

Chanjo hiyo imebainika kuwa na ufanisi kwa asilimia 78 dhidi ya COVID-19 ya ukali wa aina yoyote, siku 14 au zaidi baada ya kupata chanjo ya pili.

Pia inafaa sana kwa nchi za kipato cha chini na cha kati kutokana na mahitaji yake rahisi ya kuihifadhi.
WHO ilisema takiwmu zilizopo juu ya chanjo hiyo kwa wanawake wajawazito hazitoshi kutathmini usalama au ufanisi wake kwa kundi hilo la watu, ingawa tafiti zimepangwa kufanyika zaidi.

Kumekuwa na wagonjwa karibu milioni 247 wa COVID-19 duniani kote, na zaidi ya vifo milioni 5, kulingana na takwimu za hivi karibuni za WHO.

Zaidi ya maambukizo mapya milioni tatu yameripotiwa wiki iliyopita, yakiwakilisha hali ya kuongezeka kidogo, shirika hilo lilisema katika tathimini yake ya hivi karibuni ya janga la COVID-19, ililochapishwa jana Jumanne.
Ongezeko hilo liliongozwa na ongezeko la asilimia sita la wagonjwa wapya wa kila wiki barani Ulaya, kwani kanda zingine zimeripoti kupungua au mwenendo thabiti.