Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaokufa kwa COVID-19 duniani wapungua; Burundi, Korea Kaskazini na Eritrea hazijaanza chanjo

Muhudumu wa afya akiandaa chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini Moghadishu Somalia
© UNICEF/Ismail Taxta
Muhudumu wa afya akiandaa chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini Moghadishu Somalia

Wanaokufa kwa COVID-19 duniani wapungua; Burundi, Korea Kaskazini na Eritrea hazijaanza chanjo

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO limesema idadi ya vifo vya kila wiki kutokana na ugonjwa wa Corona au COVID-19 imeendelea kpuungua na hivi sasa imefikia kiwango cha chini zaidi kwa takribani mwaka mmoja. Anold Kayanda na maelezo zaidi.

WHO inasema kitakwimu ikilinganishwa na awali idadi hiyo ya vifo 50,000 kila wiki ni ndogo lakini kiuhalisia bado ni kubwa kwa kutambua kuwa bado watu wanafariki dunia.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva,Uswisi amesema idadi ya vifo vya COVID-19 inapungua kila ukanda wa dunia isipokuwa barani Ulaya ambako nchi kadhaa zinakumbwa na wimbi jipya la wagonjwa na vifo.

“Na bila shaka, idadi kubwa ya vifo ni kubwa miongoni mwa nchi na watu ambako bado chanjo siyo rahisi kupatikana,” amesema Dkt. Tedros akiongeza “kama unavyofahau nchi 56 ambazo zilikuwa zimeenguliwa kutoka soko la chanjo za COVID-19 duniani hazikuweza kufikia lengo la kuchanja asilimia 10 ya wananchi wake hadi mwisho wa mwezi uliopita wa Septemba na nyingi ziko Afrika.”

Hata hivyo amesema nchi nyingi zaidi ziko hatarini kushindwa kufikia lengo la kuchanja asilimia 40 ya wananchi wake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu akitaja nchi kama vile Burundi, Eritrea na Korea Kaskazini ambazo hazijaanza kutoa chanjo dhidi ya Corona.

Mataifa mengine hayana chanjo za kutosha, licha ya kwamba yameanzisha kampeni za chanjo kufikia lengo.

Ni kwa mantiki hiyo amesihi nchi na kampuni zinazodhibiti usambazaji wa chanjo duniani kupatia kipaumbele jukwaa la kimataifa la kusaka na kugawa chanjo duniani, COVAX na mpango wa Afrika wa kusaka chanjo hizo, AVAT.

Amegusia pia nchi zenye mizozo na ghasia ambako ufikishaji chanjo una mkwamo akisema WHO na wadau wake wanafanya kazi na mataifa hayo ili kuimairisha uwezo wa kiufundi na kivifaa ili chanjo ziweze kusambazwa.