Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tishio la nzige Kenya bado ni kubwa lazima kuchukua tahadhari:FAO

Nzige hawa ni hatari kwa mazao shambani
UNEP GRID Arendal/Peter Prokosch
Nzige hawa ni hatari kwa mazao shambani

Tishio la nzige Kenya bado ni kubwa lazima kuchukua tahadhari:FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesema kwa kushirikiana na serikali ya Kenya wamepiga hatua kubwa kudhibiti nzige waliovamia kaunti 29 mwezi Februari mwaka huu na sasa ni kaunti chache tu ikiwemo Turkana ambazo bado zina tatizo. Lakini limeonya kwamba kubweteka itakuwa ni hatari kubwa ya kurejea kwa nzige hao. 

Katika kaunti ya Turkana Kenya wataalam wa FAO wakiwa katika helkopta wakitathimini hali ya nzige ili kuweza kuwadhibiti.  Kwa mujibu wa shirika hilo licha ya mafanikio makubwa  waliyoyapata ya kutokomeza nzige hao wa jangwani hadi sasa bado kuna tishio la kurejea tena wimbi jingine mwishoni mwa mwaka huu na hivyo wametoa wito wa kuchukuliwa tahadhari ya hali ya juu ikiwemo kujenga mfumo imara wa ufuatiliaji na uwezo wa kikanda wa kukabiliana na nzige hao endapo watazuka tena. 

Uvamizi wa nzige unaweza kuathiri uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.
Photo: FAO/Yasuyoshi Chiba
Uvamizi wa nzige unaweza kuathiri uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu.

Wizara ya kilimo ya Kenya inasema lengo lao ni kudhibiti mayai yanayoanguliwa sasa ili nzige hao wasifikie umri wa kutaga na kuongezeka idadi.Vitalis Juma ni afisa mdhibiti wa operesheni za nzige katika kaunti ya Turkana Kenya “Tulitaka kuwadhibiti haraka iwezekanavyo kabla hawajafikia hatua ya tano ya ukuaji wao na kuwa wakubwa ambao wataanza tena kuzaliana na kutaga mayai zaidi. Hivyo tunahitaji kuwadhibiti haraka sana. “ 

Udhibiti huo unafanyika kwa njia zote kuanzia angani hadi ardhini na tangu Januari hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi huu wa Agosti zaidi ya ekari 600,000 zimeokolewa kwa kudhibiti nzige hao kwenye ukanda wa Afrika Mashariki huku nzige zaidi ya bilioni tano wakiuawa. 

FAO pia imetoa mafunzo Kenya kwa mamia ya vijana wa jeshi la kujenga taifa (NYS) ambao sasa wanajitolea wakishirikiana na maafisa wa FAO na serikali kupambana na nzige hao kama sehemu ya kuimarisha uwezo wa serikali wa kufuatilia na kutokomeza kabisa wadudu hao. 

Mwakilishi wa FAO nchini Kenya Tobias Takayarasha anasema changamoto kubwa inayowakabili ni kwamba nzuge wa jangwani huja katika wimbi kubwa na endapo operesheni za kuwadhibiti zitachelewa basi wanaweza kwenda katika eneo lingine na kisha kurejea tena “Hivyo juhudi zetu kama FAO ni kuunga mkono kinachofanywa na serikali katika kaunti, kuweza kurejesha ardhi, ili kuendeleza kazi ya wakulima na hatimaye Turkana iweze kujitosheleza kwa chakula, na hilo ndilo tumaini la kila mtu.” 

FAO inakadiria kwamba kuanzia Juni hadi Desemba mwaka huu watu wengi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki hawatakuwa na uhakika wa chakula kutokana na nzige wa jangwani na sasa ukiongeza na janga la COVID-19 hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi.