Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziwa Turkana hatarini kukauka, uhai wa wanaolitegemea mashakani 

Miradi kama hii ya FAO ya kutengeneza maeneo ya kunywa maji wanyama huko Turkana nchini Kenya, ni miradi ya kuepusha mvutano kati ya wakulima na wafugaji na pia hutunza mazingira. (2011)
©FAO/Kenya Team
Miradi kama hii ya FAO ya kutengeneza maeneo ya kunywa maji wanyama huko Turkana nchini Kenya, ni miradi ya kuepusha mvutano kati ya wakulima na wafugaji na pia hutunza mazingira. (2011)

Ziwa Turkana hatarini kukauka, uhai wa wanaolitegemea mashakani 

Tabianchi na mazingira

Nchini Kenya, ziwa Turkana ambalo ni ziwa kubwa la kudumu lililoko jangwani liko hatarini kukauka na hivyo kutishia uhai wa watu zaidi ya 300,000 wanaotegemea kipato chao kutokana na maji yake.

 

Katika kijiji cha Eruth  janga la mabadiliko ya tabianchi linanyemelea wakazi wa Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya. 

Wakazi wanalazimika kudamka alfajiri kwenda kusaka maji na miongoni mwao ni Abenyo Natiir, “mume wangu alifariki dunia, na  moyo wangu uliniambia kuwa lazima tuondoke. Lakini nini kitatokea kwa wanangu? Je watafia hapa? Siwezi kuzika wanangu hapa. Kwa hiyo niliamua kuhamishia familia yangu hapa, karibu na mjini ili niweze kupata msaada.” 

Hatari ya kukauka kwa maji ya Ziwa hili inakuja wakati wakazi wa eneo hili, mwishoni mwa mwaka 2019 na mwaka wote huu wa 2020 wamekumbwa na baa kubwa la nzige wavamizi wa jangwani ambalo halijawahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 70. 

Wadudu hao wanaharibu maeneo ya mashamba na yale ya malisho ya mifugo na kuzidi kuweka hali mbaya ya hatari, “mapigo yangu ya moyo yalikwenda mbio nilipoona hawa nzige, kwa sababu wanakula chakula tunachotegemea. Tunapoenda kusaka matunda pori mitini sasa hakuna tena. Tunachofanya ni kwenda kutafuta mabaki yaliyoachwa na nzige.” 

Sasa ukame, umaskini na nzige, vimechochea utapiamlo kwa familia za Turkana ambazo takribani watu 55,000 ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kwa mujibu wa ripoti ya hali ya chakula na lishe nchini Kenya, watoto hao wanakabiliwa na utapiamlo mkali au unyafuzi, “tulizoea kunywa maziwa na kula nyama. Tungalipika chai ya maziwa na uji na kuweka maziwa. Lakini hiyo sasa ni historia. Chai ya rangi inafanya tuwe na njaa. Pengine unakula siku moja na kisha huna chakula kwa siku moja au mbili. Unaweza kukaa muda mrefu bila kula.”