Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yapeleka mrama harakati za amani, tuwe macho - Guterres

Mlinda aman wa Umoja wa Mataifa anayehudumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kwenye ujumbe wa MINUSCA akimpatia mtoto kitakasa mikono ili kujikinga na virusi vya Corona.
MINUSCA
Mlinda aman wa Umoja wa Mataifa anayehudumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kwenye ujumbe wa MINUSCA akimpatia mtoto kitakasa mikono ili kujikinga na virusi vya Corona.

COVID-19 yapeleka mrama harakati za amani, tuwe macho - Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 linapeleka mrama harakati za kupatikana kwa amani endelevu duniani.
 

Amesema hayo leo jijini New  York, Marekani wakati akihutubia mkutano wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika kwa njia ya video kujadili majanga na changamoto za kuendeleza amani duniani hivi sasa hususan wakati wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Bwana Guterres amesema pamoja na kwamba janga hilo linatishia mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana kwa shida sambamba na amani, lakini pia inachochea mizozo na hata kusababisha kuibuka kwa mizozo mingine.

Janga la Corona na hatari kuu tatu: Wananchi wanapoteza imani na serikali

Akifafanua kwa mapana Katibu Mkuu amesema duniani anaona janga la Corona linaibua hatari kuu tatu. Mosi, “mmomonyoko wa imani ya wananchi. Majanga yanadumaza imani ya wananchi kwa serikali na taasisi za umma. Fikra kwamba mamlaka zinashughulikia vibaya janga hili au haziko wazi au zinapendelea washirika wa kisiasa, vinaweza kusababisha wananchi kupoteza imani na serikali na taasisi zake.”

Wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, wakifanya usafi wa kina kwenye kambi za wakimbizi wa kipalestina ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona.
UNRWA/Yumna Patel
Wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, wakifanya usafi wa kina kwenye kambi za wakimbizi wa kipalestina ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona.

Ametaja hatari ya pili kuwa ni kukosekana kwa utulivu wa msingi wa uchumi duniani akisema kuwa hofu yake kubwa ni madhara ya muda mrefu ya kiuchumi na kijamii yakichochewa na janga la kiuchumi duniani. “Bila hatua madhubuti, ukosefu wa usawa, umaskini duniani na uwezekano wa ukosefu wa utulivu na ghasia vinaweza kuongezeka miaka na miaka,” amesema Guterres kwenye kikao hicho kilichoitishwa na Indonesia ambayo inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Agosti.

Guterres ametaja hatari ya tatu kuwa ni kudhoofika kwa misingi inayoshikilia jamii akitoa mfano wa kubinywa kwa fursa za kiraia na kufungwa kwa michakato ya kisiasa na nafasi za kisheria kwa watu kuonesha machungu yao. Tumeshuhudia maandamano mengi ya amani, n anchi nyingi zimetumia COVID-19 kama kisingizio cha misako ya kibabe na ongezeko la ukandamizaji unaofanywa na serikali. Takribani nchi 23 zimeahirisha chaguzi za kitaifa au kur aza maoni na idadi maradufu ya hiyo zimeahirisha chaguzi za kimajimbo.”

Hata hivyo kuna fursa ndani ya hatari hizo

Guterres amesema kuwa licha ya hatari hizo bado kuna fursa a kujenga amani akigusia ombi lake la mwanzoni mwa mwaka huu la kutaka nchi zisitishe mapigano ili kutoa fursa ya kukabiliana na COVID-19 akisema kuwa, “nchi kadhaa na vikundi visivyo vya kiserikali waliitikia wito.  Pande kadhaa kinzani zilichukua hatua kupunguza mapigano au kusitisha mapigano. Lakini cha kusikitisha, katika matukio mengi, janga la Corona halikuwa sababu kwa pande kinzani kusitisha chuki au kukubaliana kusitisha mapigano.”

Amesema angalau azimio la mwezi uliopita namba 2532 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitaka sitisho la mapigano na kumalizwa kwa chuki akisema ni mwelekeo mzuri, lakini hatua zaidi zinahitajika kubadili maneno kuwa vitendo.
Ni kwa mantiki hiyo amependekeza mambo manne ya kubadili mwelekeo wa sasa wa COVID-19 kuhatarisha zaidi amani akisema mosi, “hatua zetu dhidi ya majanga lazima zitambue utete wa mizozo, kwa kufanya uchambuzi mpana ambao unaangalia ni kwa vipi janga linaathiri hatari zilizopo ambazo zinachochea mizozo.”

Pili, amesema ni ujumuishwaji ni kitu muhimu sana katika kuandaa hatua za kibinadamu na kimaendeleo wakati wa kukabiliana na janga.

Ametaka ujumuishwaji wa jamii mbalimbali, wanawake, vijana na vikundi vilivyo pembezoni kwa lengo la kujenga kuaminiana na utangamano wa kijamii.

Wanawake viongozi washerehekea baada ya kufungwa kwa warsha ya uwiano na kutatua mizozo JUba nchini Sudan Kuisni.
UNMISS
Wanawake viongozi washerehekea baada ya kufungwa kwa warsha ya uwiano na kutatua mizozo JUba nchini Sudan Kuisni.

Hatua ya tatu ni uratibu thabiti baina ya wadau wa kibinadamu, maendeleo na amani akisema ni muhimu sana katika kuwa na amani endelevu. “Kwa mfano, kuendeleza amani, tunahitaji kuhakikisha kuwa changamoto zote za kibinadamu zinashughulikiwa kwa kina na kwa njia thabiti. Lebanon ni mfano mmoja. Tujenge pia ubia thabiti na serikali, mashirika ya kikanda na sekta binafsi na mashirika ya kiraia,” amesema Katibu Mkuu.

Hatua ya Nne ni kuwa lazima kwenda na wakati na hali iliyopo ili kukidhi mahitaij ya ujenzi wa amani hasa wakati wa janga. Ametolea mfano mfuko wa ujenzi wa amani ambao amesema umebadili kazi zake mashinani katika kuwezesha kusaidia harakati dhidi ya COVID-19 kwa kusaka njia za kujenga uhusiano na jamii, kukabili kauli za chuki, kupunguza unyanyapaa na kuimarisha ujumuishaji.

Amekumbusha kuwa duniani hivi sasa, macho na masikio ni kwa viongozi ikiwemo Baraza la Usalama ili kushughulikia janga la sasa kwa njia ambazo zitakuwa na mchango chanya na wenye maana kwa maisha ya watu.