Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia migogoro ni kiini cha amani ya kudumu :Guterres

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Kutengwa, kukosekana kwa usawa na migogoro chini ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Kutengwa, kukosekana kwa usawa na migogoro chini ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Kuzuia migogoro ni kiini cha amani ya kudumu :Guterres

Amani na Usalama

Kuzuia migogoro ndio nguzo kuu ya kuhakikisha amani ya kudumu duniani amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama hii leo mjini New York Marekani uliojikita katika mada ya “amani na usalama kupitia njia za kidiplomasia za kuzuia migogoro.” 

Katibu Mkuu amesema “Kuzuia ndilo lengo kuu la kazi ya Baraza hili na maazimio yako ya kusaidia nchi kujenga amani na utulivu, na kusuluhisha mizozo yao kabla ya kuingia kwenye migogoro ya silaha. Na kuzuia migogoro ndio sababu ya kuendelea kuwepo kwa Umoja wa Mataifa.” 

Ameongeza kuwa kwa miaka 76, mfumo wa Umoja wa Mataifa umeipa dunia makao ya mazungumzo, zana na mbinu za kutatua mizozo kwa njia ya amani. 

“Ndiyo maana niliweka ajenda ya kuzuia mizozo kama kitovu cha majukumu yangu kwa awamu yangu ya kwanza na ya pili kama Katibu Mkuu. Nilitoa wito wa kuongezeka kwa diplomasia kwa ajili ya amani, ili kuhakikisha kwamba suluhu za kisiasa zinasalia kuwa chaguo la kwanza na la msingi kusuluhisha mizozo.” 

Amesema na hili linajumuisha mapitio ya zana zote zinazojumuisha usanifu wa amani wa Umoja wa Mataifa, na ushirikiano bora wa kuzuia na kutathmini hatari katika maamuzi ya Umoja wa Mataifa. 

Mbinu za kuzuia migogoro 

Katibu Mkuu ameliambia Baraza la Usalama kwamba mbinu hizo zinajumuisha uvumbuzi zaidi na mtazamo zaidi ikiwa ni pamoja na mfumo thabiti zaidi wa mapitio ya kila mwezi ya maeneo ya hatari, kufanya maamuzi ya juu na msaada mkubwa kwa nchi wanachama katika kudhibiti na kushughulikia hatari za mgogoro. 
  
Pili amesema zinajumuisha kubaini sababu na vichochezi vyote vya migogoro ikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa usawa na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu historia imeonyesha kwamba migogoro haitokei bila sababu wala haziepukiki. 
  
Ameongeza kuwa “mara nyingi, huwa  ni matokeo ya mapungufu ambayo yanapuuzwa au kutoshughulikiwa vizuri. Mapungufu katika upatikanaji wa mahitaji ya msingi kama vile chakula, maji, huduma za kijamii na dawa, mapungufu katika mifumo ya usalama au utawala ambapo vikundi vilivyodhulumiwa vinaweza kuungana na kutafuta njia ya kuingia madarakani kwa nguvu.” 
  
Zaidi ya hayo ametaja pia kuwa mapungufu ya uaminifu kwa serikali, katika taasisi na sheria, na kwa kila mmoja. 

Mapungufu katika uvumilivu na mshikamano wa kijamii - unaotokana na ubaguzi, chuki na malalamiko ya zamani na mapya. 

“Au mapungufu katika usawa kati ya matajiri na maskini, kati na ndani ya nchi, na kati ya wanaume na wanawake. Mapengo haya yote yanaweza kuwa nuru ya vurugu na hata migogoro.” 

Guterres amesisitiza kwamba “kuzuia ni suala la kusimamisha vita na migogoro kabla ya kutokea. Kutuliza kupitia mazungumzo hasa mivutano inayozua mgawanyiko na vita ambayo vinaweka mamilioni ya maisha hatarini kila siku. 
  
Lakini kuzuia pia ni suala la kuhakikisha kuwa hakuna mama anayelazimika kushinda njaa ili kulisha watoto wake.” 

Kuzuia migogoro huleta matumaini 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameainisha kwamba kuzuia migogoro ni “kuleta matumaini ya maisha bora ya baadaye kupitia elimu, huduma za afya na uwezekano wa kipato. Kukuza uvumilivu, uaminifu, usawa na heshima kwa haki za binadamu - viungo vyote vya jamii yenye amani, kuziba mapengo ya maendeleo yanayosababisha migogoro, na kuleta uhai wa ahadi ya malengo ya maendeleo endelevu kwa watu wote kwa usawa, pia kurudisha nyuma mzunguko mbaya wa migogoro na migawanyiko  na badala yake, kuanzisha mzunguko mzuri wa maendeleo na amani. Na kwa hili diplomasia ina jukumu muhimu katika kuendeleza mbnele mzunguko huu mzuri.” 
 
Hata hivyo Guterres amesema pamoja na mafanikio katika suala la kuzuia migogoro dunia haipaswi kubeteka “Ingawa tunajivunia kazi yetu, tunajua pia kwamba lazima tufanye mengi zaidi ili kuungana na juhudi zetu za kibinadamu, amani na maendeleo. Hii inamaanisha uwekezaji wa haraka katika huduma za afya kwa wote, ulinzi wa jamii, na elimu na bila shaka, chanjo za COVID-19 kwa wote. Inamaanisha kufanya kazi kukomesha ukosefu wa usawa ambao unanyima baadhi ya makundi ya watu kupata maisha bora ya kiraia na fursa za kiuchumi.” 

Pia amesema inamaanisha, hatimaye, kuhakikisha kwamba tunasawazisha mizani ya madaraka na ushiriki kwa usawa wa wanawake. 

Na inamaanisha kubadilisha ahadi yetu kwa haki za binadamu kutoka kwenye maneno hadi matendo katika kila muktadha. Hii ni muhimu ili kuzuia migogoro. 
  
Lakini pia inamaanisha kuimarisha zana zote za diplomasia za kuzuia mizozo kwa siku zijazo, kama inavyopendekezwa katika ajenda ya amani. 
  
Hii inamaanisha mifumo thabiti ya kutoa maonyo ya mapema na zana za kimkakati za utabiri utabiri wa hali ya hewa zikijumuisha takwimu bora na uchanganuzi ili tuweze kukuza uelewa wa pamoja wa vitisho ili kugundua na kuzuia majanga yanayokuja. 

Inamaanisha uwezo thabiti wa upatanishi mstari wa mbele wa juhudi zetu za kidiplomasia kujenga amani katika jamii kote ulimwenguni. 

Inamaanisha kupanua wigo wa kundi la viongozi wanawake ili watumike kama wajumbe au wataalamu wa upatanishi kama vile ambavyo tumeongeza idadi ya wanawake walinda amani na wanawake wanaoongoza operesheni zetu. 

Na inamaanisha kazi ya pamoja zaidi katika familia ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na tume ya kujenga amani kuleta pamoja utaalam wa mfumo mzima kupitia ripoti za kawaida na mazungumzo. 

Amehitimisha kwa kusema kwamba “amani ya kudumu na endelevu inataka kuwepo kwa kazi thabiti na viongozi imara, jumuiya na wabia ili kujenga utulivu ambao ni maendeleo jumuishi. Ujumbe wangu kwa Baraza hili na kwa nchi zote wanachama ni huu simama nasi tunapotafuta kujenga amani na maendeleo kupitia mazungumzo na ushirikiano. Hii ndiyo njia pekee endelevu kwa mustakabali wetu wa pamoja.