Ni wakati wa kugeuza maneno kuwa vitendo kusitisha uhasama:UN

3 Aprili 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wito wake wa kimataifa alioutoa wiki iliyopita wa kusitisha uhasama umepokelewa vyema kote duniani lakini ameonya kwamba kuna pengo kubwa kati ya azma na uteekelezaji na kusisitiza kwamba ili kunyamazisha silaha ni lazima kupaza sauti kwa ajili ya amani na kugeuza maneno kuwa vitendo.

Guterres ametoa kauli hiyo hii leo siku kumi tangu alipotoa wito wa kimataifa wa kusitisha uhasama katika ripoti yake aliyoiwasilisha kwa njia ya video mjini New York Marekani. Ameshukuru kwamba debe alipopiga limesikika katika sehemu mbalimbali zenye mogogoro lakini anahisi kwamba sasa umewadia wakati wa wito huo wa maneno kuwa vitendo

“Kuna pengo kubwa kati za maazimio na vitendo, kati ya kutafsiri maneno kuwa amani mashinani na katika Maisha ya watu. Kuna changamoto kubwa ya utekelezaji ukizingatia kwamba migogoro imedumu kwa muda mrefu , hali ya kutoaminiana imemea mizizi na shuku na shaka zikitawala.Tunafahamu kwamba mafanikio yoyote yanayopatikana ni tete na yanaweza kugeuka kirahisi na baadhi ya migogoro hata imeshika kasi zaidi. Tunahitaji hatua Madhubuti za kidiplomasia kukabili changamoto hizi. Ili kunyamazisha silaha ni lazima tupaze sauti kwa ajili ya amani.”

Uungwaji mkono wa wito huo

Guterres amesema nchi wanachama takriban 70 kufikia leo wameidhinisha wito huo lakini pia wadai wa kikanda, wanaharakati wasio wa kiserikali, mitandao ya asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa, wajumbe wote wa amani wa Umoja wa Mataifa na watetezi wa malengo ya maendeleo endelevu. Ameongeza kuwa hata viongozi wa kidini akiwemo Papa mtakatifu Francis ameongeza sauti yake kuunga mkono usitishwaji uhasama kimataifa sambamba na wananchi mbalimbali kupitia uhamasijaji mtandaoni.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mbali ya hayo wahusika wengi wamesikia wito huo ikiwemo Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Colombia, Libya, Myanmar, Ufilipino, Sudan Kusini, Syria, Ukraine na Yemen. Amesema kila mmoja akitimiza wajibu wake kuna matumaini ya amani duniani. 

“ Natoa wito kwa wale wote ambao wanaweza kuleta mabadiliko kufanya hivyo, kuwataka na kuwapa shinikizo wapiganaji kote duniani kuweka chini silaha zao. Kuna fursa kwa ajili ya amani , lakini tuko mbali kuifikia na haj ani ya haraka. Virusi vya Corona, COVIDI-19 sasa vinakuja katika maeneo haya ya vita, virusi hivyo vimedhihirisha jinsi gani vinaweza kusafiri haraka nje ya mipaka kuathiri nchi na kupindua Maisha. zahma mbaya zaidi inakuja na hivyo tunahitaji kufanya kila linalowezekana kufilkia amani na umoja ambao dunia yetu unautaka haraka ili kuweza kukabiliana na COVID-19. Ni lazima tukusanye nguvu zote katika kuushinda ugonjwa huu.”

Kwingineko vita hata vimeshika kasi

Katibu Mkuu amesema anaelewa kwamba katika maeneo mengine ambako hali ni mbaya mapigano hayaathirika vyovyote na baadhi ya migogoro hata imeshika kasi zaidi. Amesema wawakilishi wake ana wajumbe wake maalum na katika mazingira mengine waratibu wakazi wa umoja wa Mataifa wanawasiliana na wakiganaji ili kufikia muafaka wa usitishaji mapigano. Ametolea mfano wa juhudi za kidiplomasia zilizofanyika Yemen, Syria, Libya na Afghanistan.

“Katika mazingira yote haya magumu natoa wito kwa nchi ambazo zina ushawishi kwa wapiganaji kujitahidi kadri wawezavyo kufanya usitishaji mapigano kuwa hali halisi”

Lengo kwa sasa ni kuhakikisha amani

Bwana Guterres amesema lengo lake kubwa ni hakikisha amani inadumishwa “Lengo langu hivi sasa ni kuhakikisha usitishaji wa mapigano, wale ambao kimsingi waliafikiana kupitia wawakilishi wa pande zote mbili  lakini hawajatia saini, muafaka huo unatekelezwa. Ni lazima tusitishe vita hivi. Vita hivi vimekuwa na athari kubwa za kiuchumi na kijamii kwa nchi, vimewafanya watu kuteseka vibaya, na vita hivi sasa haviruhusu hatua za kukabiliana na COVID-19 kufanyika nchini Libya, hali ambayo inaweza kuwa na athari mbaya sana pia. Huu ni wakati wa kukomesha vita na ombi langu sio tu kwa pande kinzani lakini kwa wote ambao wanahusika moja kwa moja au kwa njia nyingine kwenye mzozo wa Libya kuelewa kwamba huu ni wakati wa kuvikomesha vita hivyo. Haikubaliki kidhamira kuendelea na vita hivi.”

Katimu mkuu ameongeza kuwa usitishaji uhasama ni fursa ya kidiplomasia kwa ajili ya amani, usitishaji mapigano ni fursa kwa majadiliano ya kisiasa, usitishaji uhasama ni fursa kwa hatua inayofuata kuelekea amani ya kudumu na hivyo usitishaji uhasama una thamani ya kuepusha watu kufa na kuruhusu kupamana ipasavyo na ugonjwa wa Corona, lakini usitishaji uhasama ni lazima uonekane kama hatua ya kwanza kuelekea amani ya kudumu.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter