Ninalaani vikali mashambulio dhidi ya raia bonde la ziwa Chad:Guterres

4 Agosti 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio ya kikatili dhidi ya raia katika jimbo la Lake Chad na jimbo la Kaskazini la Cameroon.

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu usiku na msemaji wake Katibu Mkuu amesema mnano tarehe 31 Julai lilifanyika shambulio kwenye jimbo la Lake Chad na tarehe 2 Agosti likafanyika shambulio lingine kwenye jimbo la Kaskazini mwa Cameroon yote dhidi ya raia na yamesababisha mauaji na kutekwa kwa raia wengi wakiwemo wanawake, watoto na wakimbizi wa ndani waliokimbia machafuko makwao. 

Duru za Habari zinasema takriban watu 10 waliuawa jimboni Lake Chad na wengine 7 kujeruhiwa huku nchini Cameroon kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani watu 18 wameuawa na mashambulizi hayo yakidaiwa kufanywa na wapiganaji wa Boko Haram.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu imetaka wote waliohusika na ukatili na uhalifu huo wawajibishwe na kusistiza kuwa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu lazima ziheshimiwe kikamilifu na raia wote nchini Cameroon na Chad lazima walindwe. 

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kusimama imara katika msaada wake kwa bonde la ziwa Chad hasa katika juhudi za kukabiliana na janga la ugaidi na kushughulikia masuala ya usalama, kisiasa, kibinadamu na changamoto za kijamii na kiuchumi katika ukanda huo. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter