Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Burkina Faso na Benin kwa kufuta adhabu ya kifo- UNOWA

Mkazi wa kijiji cha Dan Kada, eneo la Maradi nchini Nigera ambako mara kwa mara magaidi huwashambulia na kukwamisha shughuli zao za maendeleo.
UN /WFP/Phil Behan
Mkazi wa kijiji cha Dan Kada, eneo la Maradi nchini Nigera ambako mara kwa mara magaidi huwashambulia na kukwamisha shughuli zao za maendeleo.

Heko Burkina Faso na Benin kwa kufuta adhabu ya kifo- UNOWA

Amani na Usalama

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa nchi za Afrika Magharibi, Mohammed Ibn Chambas amesema licha ya harakati za kidemokrasia kuendelea kushamiri kwenye ukanda huo lbado vikundi vya kigaidi vimeendelea kuwa tishio kwenye ukanda wa Sahel na bonde la ziwa Chad.

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja huo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama jijini New York, Marekani hii leo, Bwana Chambas amesema mbinu zao za mashambulizi zinazidi kutia hofu akitolea mfano shambulio la hivi karibuni ambapo askari kutoka Nigeria waliuawa.

“Ugumu wa mashambulio ya hivi karibuni ni jambo linalotia hofu juu ya kuendelea kuugana kwa vikundi vya kigaidi vya Afrika Magharibi na vile vya waislamu wenye misimamo mikali,” amesema Bwana Chambas.

Amezungumzia pia masuala ya uchaguzi akisema wanapongeza dhima wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, jumuiya ya madola na Muungano wa Ulaya katika kupunguza mvutano wakati wa chaguzi huko Guinea, Gambia na Sierra Leone.

Amegusia pia  habari njema huko Benin na Burkina Faso ambako wamefutilia mbali adhabu ya kifo.

Doria ikiendelea kwenye mitaa ya mji wa Menaka, kaskazini mwa Mali. Msafara unajumuisha maafisa polisi wa UN, UNPOL na walinda amani kutoka Togo waliopo kwenye ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA.
MINUSMA/Marco Dormino.
Doria ikiendelea kwenye mitaa ya mji wa Menaka, kaskazini mwa Mali. Msafara unajumuisha maafisa polisi wa UN, UNPOL na walinda amani kutoka Togo waliopo kwenye ujumbe wa UN wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA.

“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu  hali ilivyo kwenye nchi ambazo zitakuwa na chaguzi hivi karibuni ambazo ni Mauritania, Nigeria na Senegal.

Mzozo wa kisiasa huko Togo nao tayari  umesababisha kusitishwa kwa uchaguzi wa bunge ambao ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka huu wa 2018,” amesema Mkuu huyo wa UNOWA.

Hata hivyo amekaribisha hatua ya ECOWAS ya kuongoza maridhiano ili hatimaye mkwamo  huo wa kisiasa Togo uweze kuondolewa kwa amani.

Bwana Chambas katika ripoti hiyo ambayo huwasilishwa mbele ya Baraza la Usalama kila baada ya miezi mitatu amegusia pia  habari njema huko Benin na Burkina Faso ambako wamefutilia mbali adhabu ya kifo, na hivyo kufanya eneo hilola Afrika Magharibi kuwa nan chi 9 ambazo zimeondokana na adhabu hiyo.