Nchi za Amerika Kusini na Karibea sasa ni kitovu cha janga la COVID-19, zisaidiwe-Guterres

9 Julai 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa kuzindua  tamko la kisera kuhusu madhara ya corona au COVID-19 kwa eneo la Amerika Kusini na Karibea ameisihi jumuiya ya kimataifa kuzisaidia nchi za ukanda huo ili zisitetereke zaidi.

Kabla ya kueleza baadhi ya mambo yanayopaswa kufanyika ili kuziokoa nchi hizo zinazoendelea kuathirika, Bwana Guterres anaeleza hali ilivyo Amerika Kusini na Karibea,

 “Wakati COVID-19 ikiendelea kusambaa kote duniani, Amerika Kusini na Karibea zimekuwa kitovu cha janga hili. Katika mazingira ambayo tayari kuna pengo la usawa, viwango vya juu vya ajira zisizo rasmi na huduma duni za afya, wengi walioko hatarini na hata mtu mmoja mmoja, kwa mara nyingine wameathirika zaidi. Wanawake, ambao ndio wanaunda nguvu kazi kubwa zaidi katika sekta ya uchumi wakiwa ndio waathirika zaidi, sasa wanalazimika kubeba dhamana ya ziada ya kulea. Na wazee na watu wenye ulemavu wako katika hatari zaidi ya kufariki dunia kutokana na virusi.”

Kuhusu nini kifanyike, Bwana Guterres amesema kunatakiwa kufanyika kila linalowezekana kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona na kudhibiti madhara ya kiafya ya janga hili, kisha akaongeza,

“Natoa wito kwa ajili ya kiasi cha fedha kuokoa na kurejesha hali ambacho ni sawa na zaidi ya asilimia 10 ya uchumi wa dunia. Nchi zilizoendelea zinafanya zenyewe kwa kutumia rasilimali zake. Kwa nchi za Amerika Kusini na Karibea, jumuiya ya kimataifa lazima itoe ukwasi, msaada wa kifedha na unafuu wa madeni. Nchi za Amerika Kusini na Karibea hususani mataifa yanazoendelea ya visiwa vidogo hayapaswi kuachwa katika msaada wa kidunia. Mwitio wa pamoja wa kimataifa unahitaji kupanuliwa hadi kwa nchi za kipato cha kati.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter