Ndege ya kwanza ya UN iliyosheheni msaada wa COVID-19 kuondoka leo kuelekea nchi za Afrika:WHO/WFP/AU

14 Aprili 2020

Ndege ya kwanza ya mshikamano ya Umoja wa Mataifa inatarajiwa kuondoka leo mjini Addis Ababa Ethiopia kuelekea nchi mbalimbali za Afrika ikiwa imesheheni msaada na vifaa ya kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona au COVID-19.

Mzigo huo wa msaada uliotolewa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, umesafirishwa kwa kushirikiana na shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP na miongoni mwa msaada uliobebwa ni “barakoa, glavu, miwani ya kitabibu, magauani ya wahudumu wa afya, vifaa vya kujikinga, mashine za kupima joto la mwili na mashine za kusaidia kupumua.”

Ndani ya ndege hiyo kuna sehemu pia ya msaada uliotolewa na waziri mkuu Abiy Ahmed na wakfu wa Jack Ma ili kusaidia kudhibiti COVID-19 barani Afrika.

Kwa upande wake Muungano wa Afrika AU, kupitia kituo chake cha kudhibiti magonjwa (Africa CDC) inatoa msaada wa kiufundi na kuratibu ugawaji wa msaada huo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley “Ndege zote za biashara zimesitishwa na ndege yenye msaada wa kitabibu imekwama. Tunaweza kukomesha virusi hivi katika chimbuko lake lakini tunapaswa kushirikiana kwa Pamoja. WFP imedhamiria kufikisha vifaa muhimu vya kitatibu kunakohitajika na kuwakinga wahudumu waa afya wakati wakiokoa maisha. Safari zetu za ndege zinapaswa kufadhiliwa kikamilifu ili kuwezesha hili na tuko tayari kusafirisha wahudumu wa afya na vifaa vya kitabibu.”

Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya

Wasomaji wanaeza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus amesema “Ndege ya mshikamano ni sehemu ya juhudi kubwa za kusfirisha vifaa vya kitabibu vya kuokoa Maisha kwa nchi 95 duniani. Napenda kuushukuru Muungano wa afrika , serikali ya Emarati na Ethiopia , wakfu wa Jack Ma na washirika wote kwa mshikamano wao na nchi za Afrika wakati huu muhimu katika historia”

Vifaa vilivyomo katika ndege ya mshikamano

Shehena hiyo  muhimu ya WHO inajumuisha “barakoa milioni moja Pamoja na vifaa vingine vya kujikinga ambavyo vitatosheleza kuwalinda wahudumu wa afya wakati wakiwatibu zaidi ya wagonjwa 30,000 barani Afrika na pia ina vifaa vya maabara ambavyo vitasaidia ufuatiliaji na utambuzi wa wagonjwa.”

Kuna upungufu wa vifaa tiba katika maeneo mengi kote duniani.
UN Photo/Loey Felipe
Kuna upungufu wa vifaa tiba katika maeneo mengi kote duniani.

Akizungumza kwa niaba ya AU mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Faki Mahamat amesema “ Muungano wa Afrika unathamini juhudi za washirika wetu WHO, WFP, wakfu wa Jack Ma, na waziri mkuu Abiy Ahmed katika kusaidia mkakati wa bara la Afrika kwa ajili ya kupambana na COVID-19. Vifaa hivi vya afya vinahitajika sana katika wakati huu muhimu ambapo vifaa tiba vimekuwa haba duniani kote. Muungano wa Afrika utaendelea kutoa uratibu utakaohitajika pampja na rasilimali ili kuhakikisha nchi wanachama wetu wanaweza kukidhi mahitaji kwa ajili ya huduma za afya wakati wa mlipuko huu.”

Akisisitiza umuhimu wa kuwalinda wahudumu wa afya katika milipuko ya magonjwa kama COVID-19 mkutugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “Tumeshuhudia mara nyingi wahudumu wetu wa afya wakiwa waathirika wa magonjwa ya kuambukiza wakati wakifanyakazi hospitali na wakati mwingine wanapoteza maisha. Hili halikubaliki, hivyo vifaa hivi vya kujikinga vitasaidia kuwalinda wahudumu hawa muhimu. WHO imedhamiria kuwalinda wale walio msitari wa mbele katika kutoa huduma za afya.”

Ndege ya mshikamano ya UN ikitokea Addis Ababa, Ethiopia itawasilisha vifaa tiba nchi kadhaa barani Afrika.
WFP/Edward Johnson
Ndege ya mshikamano ya UN ikitokea Addis Ababa, Ethiopia itawasilisha vifaa tiba nchi kadhaa barani Afrika.

Juhudi zinazofanyika

 Kituo cha WHO cha kiufundi kilichopo Dubai kikiwa na timu ya watu saba kimekuwa kikifanyakazi usiku na mchana kuhakikisha kinasafirisha shehena 130 na vifaa vya maabara kwa nchi 95 katika kanda zote sita za WHO.

Mkurugenzi wa Who kanda ya Mediterranea Mashariki Dkt. Ahmed Al-Mandhari  amesema “Shukrani sana kwa serikali ya Emarati kwa ukarimu wake kwenye operesheni hii, kituo cha kiufundi cha WHO Dubai kimefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba vifaa hivi vinatayarishwa na kusafirishwa kwenda vinakohitajika zaidi. Huu ni usafirishaji mkubwa zaidi tangu kuanza kwa mlipuko wa COVID-19 na utahakikisha kwamba watu wanaoishi katika nchi ambazo zina mifumo duni ya afya wanaweza kupimwa na kutibiwa huku ikihakikishwa kwamba wahudumu wa afya walio msitari wa mbele kupambana na COVID-19 wanalindwa.”

Asante wote waliofanikisha hili

 WHO na WFP wameishukuru serikali ya Ethiopia ambayo imeisaidia WFP kuanzisha kituo cha safari za ndege cha masuala ya kibinadamu mjini Addis Ababa wiki hii ambacho kitasaidia kusafirisha vifaa vya kujikinga, vifaa tiba na wahudumu wa kibinadamu kote barani Afrika kwa ajili ya kukabiliana na COVID-19 lakini pia kuhakikisha wahudumu wa afya wanaweza kusafirishwa endapo wnaumwa wakati wowote.

Hivi sasa kuna timu watu 25 wafanyakazi wa anga na kiufundi wa WFP wako katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa wanahusika na operesheni ya saa 24.

Pia ndio wanaohusika na ghala na shehena inayowasili na uhifadhi wa shehena hiyo na kisha kuisafirisha kwa njia ya anga.

Kwa kushirikiana na Afrika CDC WFP inafiatilia shehena zinazosafirishwa, kudhibiti kituo hicho kipya mjini Addis na kutoa huduma kwa nchi za afrika.

Mkurugenzi wa Afrika CDC John Nkengasong amesema “Vifaa hivyo vya tiba vimekuja wakati muafaka wakati bara hilo likiwa bado na fursa ya kupambana na mlipuko wa COVID-19. Hatua za Pamoja na za haraka zinatiwa shime na ndege hii ya mshikamano na hili ni muhimu sana.”

Kama sehemu ya ombi la kimataifa la kukusanya dola bilioni 2 kwa ajili ya vita dhidi ya COVID-19 limezinduliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA 25 Machi. WFP imetoa wito wa dola milioni 350 ili kuanzisha kituo muhimu cha masuala ya kibinadamu kote duniani kwa ajili ya kuwezesha uhifadhi na kusafirisha shehena muhimu za vifaa tiba, kufanya safari za ndege  kusafirisha shehena na wahudumu wa afya nah ii inajumuisha ndege ya mshikamano inayoondoka leo mjini Addis Ababa.

Hadi sasa WFP imepokea asilimia 24 sawa na dola milioni 84 kati ya dola milioni 350 inazohitaji

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter