Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yahitaji dola bilioni 1.9 kusaidia mamilioni kwa chakula wakati wa COVID-19

Vifaa tiba vilivyosambazwa na shirika la mpango wa chakula duniani nchini Panama kusambazwa katika ukanda huo.
WFP
Vifaa tiba vilivyosambazwa na shirika la mpango wa chakula duniani nchini Panama kusambazwa katika ukanda huo.

WFP yahitaji dola bilioni 1.9 kusaidia mamilioni kwa chakula wakati wa COVID-19

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema kipaumbele chake cha kwanza kwa sasa mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 ukiendelea ni kuhakikisha chakula na lishe kwa watu milioni 87 kwa mwaka huu wa 2020.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis shirika hilo limesema sasa linataka kuweka akiba ya chakula ama fedha taslimu zitakazowasaidia kutoa msaada wa chakula kwa takribani miezi mitatu kwa watu wasiojiweza kwenye nchi ambazo ni kipaumbele cha WFP. Elisabeth Byrs ni msemaji wa WFP mjini Geneva,“Tunatoa wito kwa serikali washirika kuthibitisha takribani dola bilioni 1.9 za mchango kwa program za msaada wa chakula za WFP ili kwamba ununuzi na uhifadhi wa akiba ya chakula ufanyike katika maeneo yenye matatizo.”

WFP inazitaka nchi wadau kuruhusu mabadiliko ya jinsi rasilimali zinavyoweza kutumika ili programu za msaada wa chakula ziweze kwenda sanjari na mabadiliko ya haraka yanayoendelea hivi sasa.

Fedha zaidi zinaweza kuhitajika kwa aliji ya ongezeko la msaada wa vifaa vya kimataifa kutoka kwa jamii ya masuala ya kibinadamu ikiwa itaonekana wazi kuwa janga hili la COVID-19 lina athari kubwa kwa nchi dhaifu na mifumo dhaifu ya afya na usalama.

Kilichofanyika hadi sasa

WFP imekuwa mstari wa mbele katika kupeleka msaada wakati huu mgumu wa kukabiliana na COVID-19 na tayari imeshapeleka misaada kwa nchi 67 kote duniani kwa niaba ya shirika la afya ulimwenguni WHO, ikiwemo China ambako ni kitovu cha mlipuko huo wa Corona.

Pia WFP imepeleka timu ya wataalam wake kwenye makao makuu wa WHO mjini Geneva kwa ajili ya kusaidia masuala ya kiufundi na mipango.

Nchini Iran mathalani kupitia ufadhili wa Japan imetoa vifaa vya miezi miwili vya kujikinga kama barakoa, glavu na magauni ya wahudumu wa afya.

Sehemu zingine inakotoa msaada ni pamoja na kwenye kambi kubwa ya wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh ya Cox’s Bazar, nchini Afghanistan na Zimbabwe.