Wakimbizi raia wa DRC zaidi ya 3,000 wamewasili Uganda ndani ya siku tatu

7 Julai 2020

Zaidi ya wakimbizi 3,000 raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wamewasili Uganda kati ya Alhamis na Ijumaa ya wiki iliyopita yaani Julai 1-3 wakati wa kufunguliwa kwa muda kwa vituo viwili vya mipakani, Galajo na Mlima Zeu, kaskazini magharibi mwa Uganda, limeeleza hii leo mjini Geneva Uswisi, shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi, UNHCR. 

Kwa mujibu wa mamlaka nchini DRC, wakimbizi wapya waliowasili, awali walikuwa sehemu ya kundi kubwa la takribani watu 45,000 ambao walijaribu kukimbia kuelekea katika mpaka wan chi yao na Uganda muda mfupi baada ya kutokea mapigano kati makundi ya wanamgambo jimboni Ituri tarehe 17 na 18 mwezi Mei.

Wakimbizi kutoka Congo wanajipanga kufanya uchunguzi na usalama huko Zombo, karibu na mpaka kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNHCR/Rocco Nuri
Wakimbizi kutoka Congo wanajipanga kufanya uchunguzi na usalama huko Zombo, karibu na mpaka kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

Msemaji wa UNHCR, Charlie Yaxley, akitoa taarifa hii kwa wanahabari ameeleza kuwa, “ingawa wengine wameweza kurejea katika maeneo yao ya asili, wengine walisalia karibu na mpaka wakiwa hawawezi kuvuka kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na kufungwa kwa mipaka katika upande wa Uganda ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19.”

Aidha Msemaji huyo ameeleza kuwa asilimia 65 ya kundi jipya la raia wa DRC waliowasili ni watoto. Ameeleza pia kuwa kundi jipya lilijumuishawanawake 33 wajawazito, ambapo wawili kati yao walikimbizwa haraka katika kituo cha afya cha Zeu wiki iliyopita ambako wote wawili walijifungua, mmoja akipata mtoto wa kike, na mwingine mtoto wa kiume.

“Baadhi ya wakimbizi waliwaeleza maafisa wetu kuhusu matendo mabaya yaliyotekelezwa na wanamgambo kwenye vijiji vyao. Wengi wao walitueleza kuwa walitenganishwa na familia zao na walikuwa na muda mfupi mno kukusanya mali zao au kuziangalia familia zao kabla ya kukimbia. Wachache sana walimudu kubeba vitu vyao na wengi wao walikimbia peku wakiwa na nguo tu walizokuwa wamezivaa.”  Ameeleza msemaji wa UNHCR kuhusu hali ilivyokuwa.

Wakimbizi wote waliovuka mpaka wamepelekwa katika Chuo cha kilimo cha Zeu, ambacho ni kituo cha muda mrefu cha kufundisha wakulima kilichoko katika wilaya ya Zombo na sasa kinatumika kama karantini. Ili kukisaidia kituo, UNHCR imeweka mahema 318 ya familia na pia matanki tisa ya maji, maeneo ya upimaji afya, vyoo na vyombo vya kunawa mikono. Pia UNHCR na wadau wake wanatoa chakula, maji, upimaji afya na malazi ya muda. Pia timu za wataalamu wa afya na gari la wagonjwa wako tayari ikiwa kuna yeyote atahitaji kulazwa.

Wizara ya afya ya Uganda imekuwa ikiwapima COVID-19 wakimbizi, ambapo sampuli zote 570 za mwanzo, zote zimerejea zikionesha hakuna mgonjwa kati yao. Wakimbizi wamepokea dozi za Vitamini A na chanjo dhidi ya kipindupindu, surua, rubella na polio.

Baada ya kumaiza siku 14 za kukaa karantini, wakimbizi watahamishiwa katika makazi ya wakimbizi yaliyopo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter