Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoto za vijana Uganda zatishiwa na mlipuko mpya wa COVID-19

Kutoka Maktaba: Abiria akiwa kwenye usafiri wa pikipiki maarufu kama Boda Boda mjini Kampaka nchini Uganda
© World Bank/Sarah Farhat
Kutoka Maktaba: Abiria akiwa kwenye usafiri wa pikipiki maarufu kama Boda Boda mjini Kampaka nchini Uganda

Ndoto za vijana Uganda zatishiwa na mlipuko mpya wa COVID-19

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika hivi karibuni ilionya kuwa awamu ya pili ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 barani humo itakuwa shubiri siyo tu kijamii bali kiuchumi. Nchini Uganda hali hiyo sasa ni dhahiri kwa kuwa takwimu za afya nchini humo zinaonesha  ongezeko la mambukizi kutoka watu 200 mwezi Februari mwaka huu hadi wagonjwa zaidi ya 1,000 kwa siku mwezi Mei na kuilazimu serikali kutangaza maagizo mapya ya kuudhibiti.

Maagizo yaliyotangazwa mwanzoni mwa mwezi huu ni pamoja na kufungwa kwa taasisi zote za elimu, masoko na usafiri kutoka wilaya moja hadi nyingine. Hatua hiyo imekuwa na mkwamo kwa vijana hasa wale wanaojipatia kipato kwa kusafirisha bidhaa na abiria kwa njia ya pikipiki au bodaboda. Mwandishi wetu wa Uganda, John Kibego amezungumza na vijana hao kufahamu vile ambavyo wameathiriwa na COVID-19 hivi sasa.

Katika kituo cha daladala katika mji wa Hoima, John Kibego anazungumza na kijana ambaye anajitambulisha kwa jina Tumusiime Adnan, dereva wa daladala. Kijana huyu anasema hakutarajia hali hii ya ufungaji wa mipaka kati ya wilaya na wilaya na hivyo maisha yamekuwa magumu kwake na wenzake. "Kila mtu alikuwa anafanya mipango yake akijua anaenda mbele, lakini sasa tunaanza kurudi nyuma." Anaeleza Adnan kwa masikitito.

Pia Adnan anaeleza kuwa hali ya nyumbani kwake imeanza kuwa ngumu kwani chakula kilichopo hakiwatoshi yeye na familia yake na mwaka huu alikuwa na mpango wa kujenga nyumba na pia kununua gari lake mwenyewe kwa ajili ya biashara. Kijana huyo anaeleza kuwa hali imekuwa ngumu kwa kuwa watu wameenda mashambani na wachache waliobaki mjini ni kwa kuwa hawana mahali pengine pa kwenda na hivyo usafirishaji umesimama.

Kuhusu mtazamo wake kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Coivid-19, Adnan anakiri kwamba awali watu wengine walikuwa wanadhani kuwa taarifa za uwepo wa ugonjwa ni za uongo, lakini sasa wanaamini kwani wameshuhudia watu wanaowafahamu wakifariki, "hata leo nimetoka kumzika mtu." anasema.

Mtu mwingine anayezungumza na John Kibego, ni Kiiza Mwesi almaarufu Ndombolo ya Solo, yeye ni dereva wa Bodaboda yaani pikipiki ziunazotumika kutoa huduma ya kusafirisha watu. Bwana Kiiza anasema kutokana na vizuizi, hali ya uchumi imekuwa ngumu kiasi kwamba anatoa wito kwa serikali ikiwezekana iwasaidie angalau kwa unga na maharage ili wapate kujiokoa na kusogeza siku.