Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchafuzi wa hewa utokanao na madini ya risasi umeathiri watoto Bangladesh:UNICEF

Watoto katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya, Cox's Bazar, Bangladesh wakijifunza jinsi ya kunawa vizuri  mikono
© UNICEF/Suman Paul Himu
Watoto katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya, Cox's Bazar, Bangladesh wakijifunza jinsi ya kunawa vizuri mikono

Uchafuzi wa hewa utokanao na madini ya risasi umeathiri watoto Bangladesh:UNICEF

Afya

Taarifa mpya iliyotolewa juma hili na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imebaini kwamba uchafuzi wa hewa na mazingira utokanao na madini ya risasi umeathiri  afya na akili za watoto  katika jimbo la Kathroga nchini Bangladesh.

Anik, mmoja wa watoto walioathirika kiafya na kiakili na uchafuzi wa hewa uliotokana na madini ya risasi kwenye jimbo la Kathroga Bangladesh ana umri wa miaka 8 na sasa anasumbuliwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu na kumpa changamoto hata katika usomaji wake shuleni. Karibu na nyumbani kwao kulikuwa na kiwanda cha kutengeneza betri ambacho kilighubika eneo hilo na moshi mkubwa uliojaa madini ya risasi . Sharmin ni mama wa Akin anasema,“kulikuwa na moshi mwingi uliotanda na harufu mbaya ya ajabu hewani na pia kumekuwa na kelele, tulipouliza tukaambiwa kuna kiwanda cha kutengeneza betri hapo. Majani ya miti yetu ynafunikwa na kitu kama ukungu kila asubuhi tukiamka na yanatoa harufu mbaya wakati wa usiku. Mmoja wa ng’ombe wetu alikufa na mbuzi wengi pia walikufa na sasa hatuna kitu. Akin alikutwa na kiwango kikubwa cha madini ya risasi mwili mwake zaidi ya pointi 26. Anakasirika kila wakati na kupandisha visirani kwa urahisi pia hawezi kukumbuka mambo mengi anaposoma , ameathirika vibaya na hali hii.”

Piga marufuku rangi zenye madini ya risasi
UNEP
Piga marufuku rangi zenye madini ya risasi

 

UNICEF kwa kushirikiana na mamlaka ya eneo hilo walilivalia njuga suala hilo na kutaka kiwanda hicho cha betri kinachoendeshwa kienyeji kwenye makazi ya watu kifungwe kwani athari zake ni mbaya sio tu kwa mazingira lakini kwa afya za watoto na jamii kwa ujumla. Mohammad Amzad ni mmliki wa eneo llililowekwa kiwanda hicho anasema hakujua athari zake, "mmoja wa ndugu zangu alikuwa anamiliki kiwanda cha betri nyumbani kwake na akaniambia wanataka kuendesha kiwanda hicho katika shamba langu ambalo halitumiki, sikujua kama kingeleta athari kwa afya za binadamu. Kisha kutokana na shinikozo wakalazimika kukimbia na kuacha kila kitu. Kama nitawaona tena watu kama hao kwenye shamba langu nitatoa taarifa kwa mamlaka kutokana na athari kubwa zilizojitokeza kwa watoto na mifugo, niliwaruhusu awali, asilani sintorudia tena. Nchi yetu ni masikini na gharama za matibabu ni kubwa mno hivyo najihisi vibaya sana."

Mamkala kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali  la Pure Earth na UNICEF walisafisha kabisa eneo hilo, kuondoa mabaki yote ya hatari za madini ya risasi ikiwa ni pamoja na kukwangua udongo wa juu ulioathirika na kisha kuligeuza eneo hilo kuwa na faida kwa jamii badala ya hasara kwa kupanda mbogamboga ambazo sasa zinazoisaidia jamii kwa lishe bora.