Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madini ya risasi yazidi kuharibu ubongo wa watoto duniani- ripoti

Wasichana wawili wanakata chuma kutoka kwa betri zilizotumiwa huko Dhaka, Bangladesh.
© UNICEF/Naser Siddique
Wasichana wawili wanakata chuma kutoka kwa betri zilizotumiwa huko Dhaka, Bangladesh.

Madini ya risasi yazidi kuharibu ubongo wa watoto duniani- ripoti

Afya

Mtoto 1 kati ya 3 duniani kote ana kiwango cha juu cha madini ya risasi kwenye damu yake na idadi kubwa wako nchi za kusini mwa Asia, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na mshirika wake Pure Earth.

Ripoti hiyo ya kwanza ya aina yake inasema kuwa kiwango hicho ni sawa na watoto milioni 800 duniani kote na wana mikrogramu 5 katika desilita 1 ya damu mwilini, kiwango ambacho kinahitaji hatua za haraka.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore anasema kuwa, “kutokana na dalili za mapema kuwa ni kidogo, madini ya risasi yanaharibu afya na maendeleo ya mtoto na hatimaye kifo. Kutambua uchafuzi utokanao na madini ya risasi na kuelewa madhara yake kwa maisha ya mtu na jamii, lazima kuhamasishe hatua za haraka kulinda watoto wote.”

Ripoti hiyo ikipatiwa jina Ukweli wa sumu: Watoto kuathiriwa na uchafuzi wa madini ya risasi kunatokomeza kizazi, inatokana na uchambuzi wa watoto kukumbana na madini hayo, ambapo umefanywa na taasisi ya tathmini ya vipimo vya afya, IHME.

Uchafuzi wa mazingira unaweza kuhusishwa na ongezeko la matatizo ya kiafya duniani kama saratani ya ngozi, saratani ya mapafu, pumu, sumu ya risasi, malaria, Ebola na Zika.
World Bank/Curt Carnemark
Uchafuzi wa mazingira unaweza kuhusishwa na ongezeko la matatizo ya kiafya duniani kama saratani ya ngozi, saratani ya mapafu, pumu, sumu ya risasi, malaria, Ebola na Zika.

“Madini ya risasi yanaweza kusababisha uharibifu usiorekebishika wa mishipa ya fahamu na ubongo. Yana madhara zaidi kwa watoto wachanga na wale wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa kuwa yanaharibu ubongo kabla haujakomaa, na kukwamisha maendeleo ya mtoto,”  imesema ripoti hiyo.
 
Kukumbana na madini ya risasi utotoni pia umehusishwa na afya ya akili na matatizo ya tabia na pia ongezeko la uhalifu na ghasia ambapo ripoti inaongeza kuwa, “kwa watoto wakubwa, madhara ni makubwa zaidi ikiwemo uharibifu wa figo na magonjwa ya moyo utu uzimani.”

Ongezeko la umiliki wa magari, kuchanganya na ukosefu wa miundombinu na  kanuni za kurejeleza betri zenye risasi kumesababisha ongezeko la asilimia 50 la urejelezaji wa betri hizo katika uchumi usio rasmi - Ripoti

Gharama ya madhara hayo ni kubwa zaidi kwa nchi za kipato cha chini na kati ambapo husababisha nchi hizo kupoteza takribani dola trilioni 1 kutokana na watoto ambao wangalishiriki shughuli za kiuchumi utu uzimani kushindwa kufanya hivyo.

Je ni wapi basi chanzo cha madini hayo ya risasi

Ripoti inaeleza kuwa chanzo  katika nchi za kipato cha chini na kati  ni maeneo yasiyo rasmi ya kurejeleza taka kama zile za betri za magari zenye madini ya risasi na ni kutokana na ongezeko la umiliki wa magari katika nchi hizo kuanzia mwaka 2000.

“Ongezeko la umiliki wa magari, kuchanganya na ukosefu wa miundombinu na  kanuni za kurejeleza betri zenye risasi kumesababisha ongezeko la asilimia 50 la urejelezaji wa betri hizo katika uchumi usio rasmi,” imesema ripoti hiyo.

Mathalani wafanyakazi katika mazingira hatarishi ya vituo hivyo vya kurejeleza betri za magari, vingi vyao vikiwa kinyume cha sheria, hufungua betri hizo, humwaga asidi na vumbi la risasi kwenye udongo na kisha huyeyusha risasi waliyoipata na moshi wenye sumu husambaa kwenye jamii, na mara nyingi wafanyakazi hao hawatambui madhara ya madini hayo kwenye mishipa yao ya fahamu.

Madini hayo pia huweza kuingia kwa watoto kupitia rangi za nyumba, maji yanayopitishwa katika mabomba yenye madini ya risasi, viwandani na machimbo ya madini, vikaragosi, viungo, makopo ya chakula na hata mzazi ambaye kazi zake zinahusiana na madini hayo, anaporejea nyumbani anaweza kuwa nayo kwenye nguo, nywele, viatu, na hata mikono.

Ripoti hiyo inasema kuwa, “wakati viwango vya risasi kwenye damu vimepungua kwa kiasi kikubwa katika nchi za kipato cha juu ambako hawatumii tena petroli na rangi za nyumba zenye madini hayo, hali ni tete kwa nchi za kipato cha kati na chini hata baada ya hatua za kutokomeza petroli yenye risasi duniani.”
 
Maeneo matano ambako ripoti imejikita kuonesha jinsi madini hayo na mengine yameathiri watoto ni Kathgora, Bangladesh; Tbilisi, Georgia; Agbogbloshie, Ghana; Pesarean, Indonesia; na jimbo la  Morelos, Mexico.

Hatua za kuchukua

Ni kwa mantiki hiyo ripoti ina mapendekezo matano ikiwemo kuwepo kwa mifumo ya kufuatilia na kuripoti kuhusu madini ya risasi ambapo uchunguzi wa viwango vya madini hayo kwenye damu uweze kufanyika.

Pili hatua za kuzuia na kudhibiti, tatu usimamizi na tiba, nne kuelimisha umma na kubadili tabia, tano sheria na sera na sita hatua za kimataifa na kikanda ikiwemo kuwa na kipimo kimoja cha kimataifa kuhusu kiwango cha madini hayo kwenye damu.