Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chakula ni dawa bora zaidi wakati wa mtafaruku:WFP

Wakati wa mlipuko wa COVID-19 shirika la mpango wa chakula duniani WFP linagawa msaada wa kadi za fedha kwa familia 1,500 huko El Alto na La Paz, Bolivia
WFP/Morelia Eróstegui
Wakati wa mlipuko wa COVID-19 shirika la mpango wa chakula duniani WFP linagawa msaada wa kadi za fedha kwa familia 1,500 huko El Alto na La Paz, Bolivia

Chakula ni dawa bora zaidi wakati wa mtafaruku:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mamilioni ya watu wako katika hatihati ya kutumbukia kwenye zahma ya njaa mwaka huu kwa sababu ya janga la corona au COVID-19 kwa mujibu wa shirika Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, ambalo leo limetangaza mipango ya kuboresha kwa kiasi kikubwa operesheni zake za msaada wa chakula duniani ili kuwafikia mamilioni hayo ya watu.

Akitoa tahadhari mkuu wa WFP David Beasley amesema makadirio mapya yanaonyesha kwamba watu milioni 270 watakabiliwa na tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Wasio na uhakika wa chakula waongezeka mara mbili

Kwa mujibu wa bwana. Beasley ongezeko hili ni asilimia 82 ukilinganisha na kabla ya mlipuko wa janga la COVID-19 na kuongeza kwamba virusi vya corona vimekuwa vikiathiri maeneo ambayo hapo awali yalifanikiwa kuepuka changamoto ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

“Walio msitari wa mbele katika vita dhidi ya corona hivi sasa mwelekeo unabadilika kutoka nchi tajiri na kuingia katika nchi masikini”

Hivi sasa amesema nchi za Amerika ya Kusini zinashuhudia athari mbaya zaidi za mgogoro wa kiafya kukiwa na ongezeko mara tatu la idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula.

Watu hao wanajumuisha jamii za mijini katika nchi zenye kipato cha chini na cha wastani ambako WFP imeonya kwamba “Waanatumbukia katika janga kubwa kwa wengi kupoteza ajira na kupungua kwa kiasi kikubwa fedha wanazopokea toka nje.”

Ongezeko la njaa kwa mujibu wa WFP linashuhudiwa pia katika nchi za Magharibi na Katikati mwa Afrika ambako ongezeko la watu wasio na uhakika wa chakula ni asilimia 135 na Kusini mwa Afrika ongezeko ni asilimia 90.

Hatua zinazochukuliwa na WFP

Ili kukabiliana na ongezeko hili la njaa , WFP inachukua hatua kubwa za kibinadamu katika historia ya operesheni za misaada.

Inatarajia kuwafikia na kuwasaidia watu milioni 138 kutoka milioni 97 waliosaidiwa mwaka jana.

Ili kufanikisha hilo ufadhili endelevu unahitajika haraka amesema Bwana. Beasley katika ombi alilotoa la dola bilioni 4.9 katika miezi sita ijayo ili kuzisaidia nchi 83.

“Mpaka siku tutakayokuwa na chanjo ya kitabibu, chakula ni chanjo bora dhidi za zahma yoyote. Bila chakula tutashuhudia ongezeko la machafuko ya kijamii na maandamano, ongezeko la uhamiaji, ongezeko la machafuko na kuendelea kwa utapiamlo miongoni mwa watu ambao hapo kabla walikuwa na kinga dhidi ya njaa.”