Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa ya kuchora yawa kimbilio la mkimbizi wakati wa COVID-19

Solomon Gebreyonas Alema, mkimbizi kutoka Eritrea huko Libya akitumia kipaji chake cha usanii kujipa faraja na matumaini wakati huu wa karantini ya COVID-19.
UNHCR Video
Solomon Gebreyonas Alema, mkimbizi kutoka Eritrea huko Libya akitumia kipaji chake cha usanii kujipa faraja na matumaini wakati huu wa karantini ya COVID-19.

Sanaa ya kuchora yawa kimbilio la mkimbizi wakati wa COVID-19

Wahamiaji na Wakimbizi

Kipaji na mapenzi ya uchoraji wa sanaa vimempatia mkimbizi kutoka Eritrea anayeishi nchini Libya faraja na matumaini wakati huu wa zama za janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, linalogubikwa pia na mapigano na kudorora kwa hali ya kiuchumi na kijamii katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Msanii huyo Solomon Gebreyonas Alema mwenye umri wa miaka 29, anaendeleza kipaji chake hicho ndani ya chumba kidogo cha pagala moja kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli ambako anachora na kupaka rangi.

Solomon anasema kuwa, “kuchora kuna maanisha uhai kwangu mimi, ni sehemu ya maisha yangu.”

Mkimbizi huyo amekuwa akichora picha na kuzipaka rangi tangu akiwa mdogo akisema kuwa alijifunza mwenyewe na katu hajawahi kupata mafunzo rasmi ya sanaa. Imani yake ya kikristo pia imekuwa na ushawishi mkubwa na kiasi kikubwa cha sanaa yake zina misingi ya kidini na sasa wakati huu wa karantini kutokana na COVID-19, sanaa imekuwa ndio kimbilio lake.

Watu wote wanapozali, wanapata aina fulani ya matumaini. Na kwa kutumia michoro hii ya rangi ya wakati wa kusali, watu wanaendele kutunza imani zao,”  amesema Solomon ambaye anaishi kwenye pagala lenye mwanga hafifu, likiwa na idadi kubwa ya wakimbizi wapatao 200 kutoka Eritrea, Ethiopia na Sudan.

Karantini ya COVID-19 imesababisha wengi wao kuhaha ambapo Solomon anasema kuwa, “fikra za watu zimejikita sana kwenye virusi vya Corona. Wana hofu kubwa kwa sababu watu wengi hapa maisha yao ni ya kupata na kula tu.”

Mkimbizi huyo aliondoka Eritrea na kuacha familia yake kwa lengo la kutimiza ndoto yake ya sanaa ya uchoraji na majaribio yake ya kufika Ulaya, mara kadhaa yameshindikana na sasa amekwama nchini Libya.

Solomon anasema, “nimekuwepo nchini Libya kwa miaka mitatu sasa na kitu kimoja kinachotupatia matumaini ni kuwa chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCRHatukukata tamaa kwa sababu ya shirika hilo na pia kwa sababu ya imani yetu.”

Libya imekuwa kwenye karantini ya COVID-19 tangu katikati ya mwezi Machi mwaka huu, hali ambayo inazuia wakimbizi na wahamiaji kujipatia kipato kupitia kazi za vibarua.

Hadi sasa Libya imeripoti wagonjwa 571 na kati yao hao 10 wamefariki dunia.