Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi atumia Yoga kuleta ustawi kwa wakimbizi wengine kambini Kakuma 

Kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenyal.
OCHA/Gabriella Waaijman
Kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenyal.

Mkimbizi atumia Yoga kuleta ustawi kwa wakimbizi wengine kambini Kakuma 

Wahamiaji na Wakimbizi

Msongo wa mawazo, kiwewe na matatizo mengine ya akili ni moja ya changamoto zinazowapata wakimbizi kutokana na mazingira wanamoishi au maisha waliyopitia. Kutana na Rita Brown, mkimbizi kutoka Uganda ambaye anatumia nguvu ya mazoezi ya viungo aina ya Yoga kuleta ustawi na uponyaji kwa wakimbizi walioko katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.

Rita Brown aliwasili Kakuma akitokea Uganda mnamo mwaka 2000 baada ya kuukimbia mgogoro kati ya kundi la waasi na jamii wenyeji. Rita wakati huo alikuwa na umri wa miaka 7. Baba na mama yake waliuawa. Rita anasema, “nilikuwa nikifikiri sipendwi. Nilikuwa nikifikiria kila kitu nilichopitia kilikuwa kama hatima ambayo Mungu alikuwa amenipangia, kwamba nitateseka maisha yangu yote. Lakini kwa kuwa nilijiunga na yoga, kiakili, kiroho, kihisia, nilihisi yoga kweli imenibadilisha. " 

Rita alijifunza Yoga mwaka 2019 kupitia mradi wa Afrika Yoga. Baada ya kuhitimu mafunzo hayo ambayo kwa kawaida hufanyika kwa mtu kuutuliza mwili na kutafakari, alianza kutoa mafunzo kama hayo kwa wakimbizi na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kambini hapo Kakuma. Kutokana na janga la COVID-19 amehamishia mafunzo yake mtandaoni na kuwafikia watu wengi zaidi na ujumbe wake wa kujikubali na ustawi wa akili, "ninafanya madarasa ya mtandaoni, hiyo ni Zoom na Facebook au darasa la ana kwa ana moja kwa na mtu mmoja au wawili kwa sababu ya umbai kati ya mt una mtu. Ninaipa nguvu zangu zote. Kila kitu changu ili kubadilisha maisha ya mtu ambaye ameteseka au anayeteseka. ” 

Mpango wa Rita unafanana na kipaumbele cha UNHCR kuhakikisha upatikanaji wa afya ya akili kwa wakimbizi katika kambi hiyo.  Rita anasisitiza, “yote ni kuhusu mawazo yako na jinsi unavyoyachukulia kwa sababu ikiwa una matumaini kila kitu kitakuwa chanya. "