Tunataka watambue kuwa kuna binadamu wanaojali binadamu wenzao- Catalina

Tunataka watambue kuwa kuna binadamu wanaojali binadamu wenzao- Catalina
Catalina, si jina lake halisi, ni mwanasheria kutoka Nicaragua mwenye umri wa miaka 44 na ambaye alikimbilia nchi jirani ya Costa Rica ili kunusuru maisha yake na ya watoto wake wawili.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema kuwa Catalina hivi sasa ni mkimbizi Costa Rica.
Mwaka 2018 wakati wa maandamano dhidi ya serikali nchini Nicaragua, Catalina alifungua milango ya nyumba yake ili kusaidia waandamanaji ambapo aliwapatia chakula pamoja na huduma ya kwanza pindi walipopata majeruhi.
Hata hivyo kitendo chake cha mshikamano na waandamanaji kilimfanya awe mlengwa ambapo usiku mmoja, mtu asiyefahamamika alirusha kilipuzi kupitia dirisha lake wakati wao wakiwa wamelala, ambapo kilipuzi hicho kilimjeruhi Catalina hususan eneo la mguuni.
“Mabomu mawili yalilipuka, moja kwenye mguu wangu na lingine kwenye kidevu. Nilipata vipande vidogo vidogo vya kilipuzi hicho kwenye mwili wangu, kifuani, mikononi na miguuni,” anasema Catalina akiongeza kwamba, “dole gumba la mguuni ilibidi likatwe na nilifanyiwa upasuaji mara nane pindi nilipokuwa nimelazwa, ikiwemo kupandikizwa ngozi mpya.”
Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.Kwa hofu ya maisha yake, Catalina ndipo aliamua kukimbia Nicaragua na kuingia Costa Rica licha ya kwamba majeraha bado hayakuwa yamepona na hakuweza kupata daktari.
UNHCR inasema kwamba kwa miaka kadhaa alikuwepo Costa Rica bila matibabu na kuhatarisha uwezo wa kusalia na ulemavu wa kudumu.
Ndipo aliposikia taarifa kuhusu mkataba uliotiwa saini kati ya mfumo wa hifadhi ya jamii wa Costa Rica na UNHCR wa kuwezesha wakimbizi na wasaka hifadhi walio hatarini kupata huduma bora za afya za taifa hilo la Amerika ya Kusini.
Makubaliano hayo yalitiwa saini kati ya mamlaka ya hifadhi ya jamii ya Costa Rica na UNHCR na yamewaongezea mwaka mmoja zaidi wasaka hifadhi wapatao 6,000.
María José Barth, afisa wa afya ya umma wa UNHCR anasema, “kupata huduma ya afya ni muhimu ili kuwezesha wakimbizi na wasaka hifadhi kuweza kujenga upya maisha yao kwa utu.”
Kupitia makubaliano hayo, UNHCR inatoa fedha kusaidia mpango mpya wa huduma ya afya, ambao umepatiwa umuhimu zaidi wakati huu wa janga la virusi vya Corona au COVID-19.
Janga la Corona limepiga ukanda wa Amerika na UNHCR iliibuka na mpango huo hususan kulenga watu walio hatarini zaidi wakiwemo wazee.
Wakati huu ambapo Catalina anapata ahueni, fikra zake zinarejelea kwa wale wanaosaidia raia wa Nicaragua nchini Costa Rica pamoja na kusaidia wasio na makazi akisema,“tunaziba pengo na kushughulikia mahitaji ya msingi na kuwafanya watambue kuwa kuna binadamu ambao wanajali binadamu wengine.”
Kwa mujibu wa UNHCR, takribani raia 86,000 wa Nicaragua wamesaka hifadhi nchini Costa Rica.