Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuongezeeni muda wa kurejesha mikopo, COVID-19 imetuathiri – Watu wenye ualbino

Maccelina Chuwa, mkazi wa Dodoma nchini Tanzania wakati wa mahojiano na UN News Kiswahili.
UN
Maccelina Chuwa, mkazi wa Dodoma nchini Tanzania wakati wa mahojiano na UN News Kiswahili.

Tuongezeeni muda wa kurejesha mikopo, COVID-19 imetuathiri – Watu wenye ualbino

Afya

Kuelekea siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino kesho tarehe 13 mwezi Juni, baadhi ya watanzania wenye ualbino wamepaza sauti ya kile wanachoomba kifanyike kuwanusuru wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Wamepaza sauti hizo huko Dodoma, mji mkuu wa Tanzania wakati wakihojiwa na Devotha Songorwa wa Radio washirika Kids Time FM ambapo miongoni mwao in Maiko Salali ambaye kilio chake yeye ni urejeshaji wa mikopo halmashauri.

Bwana Salali anasema kuongezwa kwa muda wa kurejesha fedha za mikopo, “ili kuweza kuwapatia watu wenye ulemavu muda wa kujiandaa vizuri, waweze kupata fedha za kurejesha. Hii ni kwa sababu kutokana na changamoto hii ya Corona, wengi wao hata zile biashara walikuwa wanafanya, zimesitishwa kufanyika. Mimi niombe serikali yangu kwamba tuone namna hizi halmashauri zinaweza kurefusha muda wa kurejesha marejesho yao, ili waweze kupata nafasi ya kujiandaa, ili waweze kurudi na kurejesha. Lakini pia niwaombe watu wenye ualbino wenyewe, katika kipindi hiki ambacho tunahangaika kurudisha uchumi wetu, tunahangaika kurudi kwenye mapamabano ya kiuchumi , tujue kwamba tuna wajibu wa kujilinda dhidi ya jua kwa kuwa jua ndio adui yetu namba moja.”.

Maiko Salali, mkazi wa Dodoma, Tanzania wakati wa mahojiano na UN News Kiswahili.
UN Tanzania
Maiko Salali, mkazi wa Dodoma, Tanzania wakati wa mahojiano na UN News Kiswahili.

Tuwapatie vifaa kinga watoto wenye ualbino

Akaenda mbali zaidi juu ya kusaidia watoto na wanafunzi wenye ualbino kujikinga na Corona pale watakaporejea shuleni na vyuoni akizitaja akisema, “shule ya Bulhangija, shule ya Mitindo na maeneo mengine yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Niwaombe watanzania kwa tunahitaji kupeleka vifaa kwenye hayo maeneo ili watoto hao wenye ulemavu wakirudi shuleni waweze kusoma kwa uhuru pasipo shida yoyote inayoweza kuleta mazingira ya wao kupata maambukizi. Kwa hiyo tunahitaji kupeleka vifaa kinga ili wajikinge.”

Maccelina Chuwa yeye anamulika matumizi ya mafuta yao akisema, “mafuta mnayotupatia, wengine hatufahamu jinsi ya kuyatumia. Mnatakiwa mtupatie elimu kwa sababu unakuta wengine anajipaka mwili mzima kuanzia usoni hadi miguuni, wengine wanasema unapata usoni na kwenye mikono, hatujui jamani, naomba elimu itolewe haya mafuta tunatumia vipi.”

Lakini akawa si mnyimi wa shukrani hasa katika kupungua kwa ukatili dihdi ya watu wenye ualbino akisema, “nashukuru serikali yetu kukomesha na kutokomeza mauaji ya watu wenye ualbino, hivi sasa mauaji yamepungua. Pia kushukuru serikali kuwa kipindi cha Albino Day bado kipo na kinasaidia watu kuzidi kutambua kuwa watu wenye ualbino ni kama watu wengine.” 

Maudhui ya siku ya kimataifa ya ualbino ni Ameumbwa kung’ara kumulika mafanikio ambayo kundi hilo limepata huku ikitoa fursa pia ya kumulika changamoto kama vile wakati huu wa COVID-19 na unyanyapaa.

Kutokana na janga la Corona, maadhimisho hayo kimataifa yatafanyika kwa njia ya mtandao ambapo mtu anayetaka kushiriki anaweza kujisajili kupitia hapa.

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
“Nasi tu binadamu” Bi. Chuwa

 

Mahojiano ya ripoti hii yamefanywa na Devotha Songorwa wa Radio washirika Kids Time FM, Dodoma.