Kutana na Emmanuel, kijana mchechemuzi wa haki za mtoto
Kutana na Emmanuel, kijana mchechemuzi wa haki za mtoto
Ikiwa leo ni siku ya mtoto duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetumia siku ya leo kuonesha ni kwa jinsi gani vijana wameamua kuchukua hatua kusongesha haki za msingi za mtoto ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.
Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema vijana hao ambao ni wachechemuzi vijana wa shirika hilo kutoka sehemu mbalimbali duniani, wanapaza sauti zao kuhusu masuala ambayo ni muhimu kwa kizazi chao na wanatoa wito kwa watu wazima kuchukua hatua ili kujenga mustakabali bora kwa wote.
“Wakati huu ambapo dunia inajikwamua kutoka janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kusikiliza sauti za vijana na watoto,” imesema taarifa hiyo.
Kutana na vijana wachechemuzi wa UNICEF
Katika kupaza sauti zao kwa ajili ya wadogo zao, mabingwa hao vijana wanaonesha njia kupitia majawabu mapya bunifu kwa changamoto zinazokabili dunia hivi sasa.
Miongoni mwao ni Emmanuel Msoka mwenye umri wa miaka 18 kutoka Tanzania, kijana mbunifu na mwanaharakati wa haki za mtoto ambaye ubunifu wake ni katika huduma za usafi na kujisafi, WASH.
Wakati wa COVID-19 shule zilifungwa na Emmanuel alikuwa na watoto yatima akiwafundisha kwa kipindi chote cha miezi mitatu masomo mbalimbali ili shule zinapofunguliwa wasiwe wameachwa nyuma. halikadhalika wakati wa janga la COVID-19, "nilibuni mashine ya kunawia mikono ili kuimarisha usafi na kusaidia kupunguza kuenea kwa virusi vya Corona.” anasema Emmanuel.
Nini kilimchochea Emmanuel?
Kichocheo cha Emmanuel katika ubunifu ni hali ya kuona yeye alibahatika kukuzwa katika familia ya baba na mama na kuona wengine wakikua bila wazazi na hivyo licha ya kwamba familia yao ilikuwa ya kimaskini, hakuchelea kupatia wasio na makazi kile kidogo alichokuwa nacho.
“Nilikua huku nikiwa na nia ya kubadilisha mambo yafanyikavyo na kutatua matatizo ya kijamii na ukosefu wa haki. Kila wakati nimejikita katika watoto na vijana kwa kuwa ndio wanaokumbwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa usawa. Hata hivyo nikagundua kuwa wengi wao hawawezi kupaza sauti zao pindi wanapokabiliwa na matatizo.” anasema Emmanuel.
Emmanuel, tangu akiwa na umri wa miaka 14 ameendesha mafunzo na semina za kujengea uwezo watoto na vijana wenzake huku akisaka mbinu za kutatua changamoto za kijamii.
“Nilikwenda kwenye karakana yangu na kuibuka na ubunifu wa mashine ya kunawa mikono ambayo inatumia pedali mbili, moja ya kuwezesha kutoa sabuni na nyingine ya kutoa maji kwenye ndoo. Nimetumia pia muda wangu kufundisha vijana na watoto wabunifu jinsi ya kuibuka na suluhu bunifu za kutatua changamoto kwenye jamii zao. Miongoni mwao ni Andrea ambaye ameshinda tuzo nyingi katika mashindano ya ubunifu wa kisayansi,” amesema Emmanuel.
Siku ya mtoto duniani ilianzishwa mara ya kwanza mwaka 1954 na huadhimishwa tarehe 20 mwezi Novemba ya kila mwaka kusongesha mshikamano wa kimataifa na uelewa wa haki za mtoto duniani kote kwa lengo la kuimarisha ustawi wa mtoto.
Tarehe 20 mwezi Novemba ni siku ambayo mwaka 1959 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliridhia azimio la haki za mtoto na pia ni tarehe ambayo mwaka 1989 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Kimataifa wa haki za mtoto, CRC.