Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP yapigia chepuo uimarishaji wa sekta ya utalii Tanzania

Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Christine Musisi akizindua moja ya magari ya wagonjwa ambayo yamebadilishwa kutoka magari ya kawaida kufuatia msaada wa fedha kutoka shirika hilo la UN.
UNDP/Sawiche Wamunza
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Christine Musisi akizindua moja ya magari ya wagonjwa ambayo yamebadilishwa kutoka magari ya kawaida kufuatia msaada wa fedha kutoka shirika hilo la UN.

UNDP yapigia chepuo uimarishaji wa sekta ya utalii Tanzania

Afya

Nchini Tanzania, shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP limeshiriki katika uzinduzi wa moja kati ya magari matatu ya magonjwa ambayo yatatumika katika hifadhi ya Taifa na mbuga za wanyama wakati huu ambapo taifa hilo la Afrika Mashariki limefungua tena milango yake kwa watalii wa nje na wa ndani.


Uzinduzi huo umefanyika jijini Arusha ambapo Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania Christine Musisi amesema, “kwa kutambua utalii kama kichocheo cha maendeleo endelevu na uwezo wake wa kuchangia katika malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, kutokana na athari zake mtambuka katika sekta na viwanda mbalimbali, sisi tuko makini kuendelea kusaidia serikali katika kuandaa mkakati madhubuti wa kuikwamua sekta ya utalii Tanzania Bara na Visiwani.”

Ujio wa COVID-19 mwezi Machi mwaka huu ulisababisha kusitishwa kwa muda kwa shughuli za utalii hadi mwezi Juni mwaka huu zilipoanza tena na watalii kuanza kuingia kutoka nje ya nchi.

UNDP ilitoa fedha kwa chama cha wapanga safari za utalii Tanzania, TATO, fedha ambazo ni za kukarabati magari matatu ili yawe magari ya kisasa ya kubebea wagonjwa.

Gari lililokabidhiwa leo lilikuwa limetolewa na mwanachama wa TATO, Tanzania Wilderness Camp.

Magari hayo ni kwa ajili ya mbuga za Serengeti, Kilimanjaro, Tarangire-Manyara na hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Fedha hizo pia zimetumika kununulia mavazi ya kukinga mwili dhidi ya COVID-19, PPE ambayo yanahitajika kwa kiasi kikubwa hivi sasa kulinda watalii na wale wanaowahudumia.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Christine Musisi (wa pili kushoto) akiwa na maafisa wa serikali na wa TATO, walitembelea karakana iliyotumika kugeuza magari hayo ya kawaida kuwa magari ya wagonjwa.
UNDP/Sawiche Wamunza
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Christine Musisi (wa pili kushoto) akiwa na maafisa wa serikali na wa TATO, walitembelea karakana iliyotumika kugeuza magari hayo ya kawaida kuwa magari ya wagonjwa.

UNDP inasema kuwa, “lengo kuu la kuwasilisha magari hayo ya wagonjwa ni kuwahakikishia watalii kuwa Tanzania imejiandaa vyema kuchukua hatua za haraka iwapo kuna dharura yoyote itatokea, ikiwa ni moja ya mipango ya kitaifa ya kuanza kukaribisha tena wageni wanaokuja nchini humu kwa mapumziko.”

Kwa kuwa mpango huo ni ule wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, “serikali itatoa wahudumu wa afya na sekta binafsi itatoa magari ya wagonjwa,” imesema taarifa ya  UNDP.

Akizungumzia msaada huo wa UNDP, Sirili Akko ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TATO amesema kuwa, “sisi katika sekta binafsi tunashukuru sana UNDP kwa msaada wao uliokuwa unahitajika sana. Msaada huu utasaidia katika kukwamua haraka sekta yetu, ambayo inachangia katika upatikanaji wa fedha za kigeni na pia ni tegemeo kwa maelfu ya biashara ndogo na pia ajira.”

 

Utalii wa mbugani unakua nchini Tanzania mwaka hadi mwaka ambapo kila mwaka watalii wapatao milioni 1.5 hutembelea taifa hilo na  kuleta mapato ya dola bilioni 2.5.

 

Halikadhalika utalii ni chanzo cha ajira 600,000 nchini Tanzania na watu wengine zaidi ya milioni moja hujipatia kipato kutokana na uwepo wa sekta hiyo.