Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yawa upenyo wa kutangaza maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama- Ripoti

Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.
© UNICEF/Zahara Abdul
Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.

COVID-19 yawa upenyo wa kutangaza maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama- Ripoti

Afya

Ripoti mpya ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau, inaonesha kuwa juhudi za kukomesha matangazo ya maziwa ya kopo kwa ajili ya watoto wachanga zinaendelea kukumbwa na mkwamo hasa wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Taarifa iliyotolewa mjini New York, Marekani na Geneva, Uswisi hii leo imesema kuwa ripoti hiyo ikiwa imeandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya WHO na mtandao wa kimataifa wa hatua kuhusu chakula cha mtoto, IBFAN, inasema kuwa maziwa ya mama yanakumbwa na vikwazo kutokana na fikra potofu ya kwamba yanaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya Corona kwa mtoto.

 WHO na UNICEF wanahamasisha mama aendelee kunyonyesha mtoto hata wakati wa janga la COVID-19, hata kama amethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anashukiwa kuwa navyo.

 Mashirika hayo yamesema kuwa, “wakati watafiti wanaendelea kuchunguza maziwa kutoka kwa mama mwenye virusi vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona, ushahidi wa sasa unadokeza kuwa hakuna uwezekano wa virusi hivyo kuambukizwa kupitia unyonyesaji au kwa kumpatia mtoto maziwa yaliyokamuliwa kutoka kwa mama mwenye virusi au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona.”

 Ripoti inasema kuwa uchunguzi kutoka mataifa 194, umebaini kuwa ni nchi 6 tu ambazo zina mikakati ya kisheria kuhusiana na kanuni ya kimataifa ya kutangaza maziwa mbadala ya mama na tatizo kubwa ni pale baadhi ya vituo vya afya vina matangazo ya maziwa ya kopo.

Kanuni hiyo inapiga marufuku aina zote za matangazo ya maziwa mbadala ya mama, ikiwemo matangazo, zawadi kwa wahudumu wa afya na mgao wa bure wa sampuli za maziwa hayo.

Kikundi cha wanawake cha kuonyeshana mshikamano katika unyonyeshaji wa watoto wao.
UN
Kikundi cha wanawake cha kuonyeshana mshikamano katika unyonyeshaji wa watoto wao.

Akizungumzia ripoti hiyo, Dkt. Francesco Branca ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula, WHO, amesema kuwa, “mikakati mizito ya matangazo ya maziwa ya unga kwa mtoto, hasa kupitia wataalam wa afya ya kwamba wazazi waamini ushauri wa lishe na afya, ni pigo kubwa katika kuimarisha afya yam toto mchanga na mtoto kwa ujumla duniani kote.”

WHO na UNICEF wanapendekeza kuwa mtoto anyonye maziwa ya mama pekee kwa miezi 6 ya mwanzo na baada ya hapo aendelee kunyonya hadi miaka 2 na zaidi huku akipatiwa vyakula vingine vyenye lishe.

Mkuu wa masuala ya lishe UNICEF, Dkt. Victor Aguayo amesema kuwa kadri janga la COVID-19 linavyozidi kuenea, wahudumu wa afya wanaelekezwa maeneo ya kusaidia kudhibiti janga hilo, huku suala la unyonyeshaji ambalo linaokoa maisha ya mamilioni ya watoto, linakosa mwongozo wa kutosha, “tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kila mama na kila familia inapata mwongozo unaotakiwa kutoka kwa wahudumu wa afya waliobobea ili waweze kunyonyesha watoto wao tangu wanapozaliwa.”

 Je mama mwenye virusi vya Corona afanyeje ?

 Ripoti inasema kuwa mama aliyethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi hivyo anaweza kuendelea kunyonyesha na kwamba wanapaswa kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji na sabuni au dawa za kutakasa mikono kabla ya kumbeba au kumshika mtoto.

 Pili avae barakoa ya kitabibu wakati akiwa amembeba au anamhudumia mtoto ikiwemo wakati anamlisha.

 Tatu apigie chafya au akoholee kwenye kitambaa kisha anawe mikono na nne, asafishe eneo mara tu anapokuwa ameligusa.