Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imebadili maisha ya familia yangu- Mwanahabari Kanyinda

Dieunit Kanyinda, mwanahabari kutoka Kinshasa, DRC akirekodi kipindi chake kutokea nyumbani.
UNICEF VIDEO
Dieunit Kanyinda, mwanahabari kutoka Kinshasa, DRC akirekodi kipindi chake kutokea nyumbani.

COVID-19 imebadili maisha ya familia yangu- Mwanahabari Kanyinda

Afya

Ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, upo na chonde chonde tujikinge. Ni kauli ya mwandishi wa habari wa kujitegemea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC aliyoitoa baada ya kupona ugonjwa huo ulioenea katika mataifa 216 duniani.

Mwanahabari huyo Dieunit Kanyinda mkazi wa mji mkuu wa DRC, Kinshasa alibainika kuwa na virusi vya Corona tarehe 13 mwezi uliopita wa Aprili ambapo alilazimika kulazwa hospitalini kwa siku 16.

Bwana Kanyinda ambaye ni baba wa watoto 5 anasema aliyopitia wakati wa kuugua kwake ni sawa na kuwa jehanam na hii leo maisha ya familia yake yamebadilika kwa kuwa “hivi sasa siwezi tena kuwabusu watoto wangu. Tunasalimia kwa mbali. Kila wakati tunajikuta katika mazingira ya tahadhari na kujikinga. Wa hiyo mambo mengi yamebadilika.”

Si tu maisha ya familia yake yamebadilika, bali pia utendaji wake wa kazi kwa kuwa hivi sasa analazimika kufanya kazi yake ya uandishi wa habari na kuchapisha video zake mtandaoni akiwa nyumbani.

Kanyinda anasema kuwa, “hapa nyumbani ni kama pahala pa vifaa vya vya redio na video. Naandaa matangazo yangu, napiga filamu ya video na kuhariri kutokea hapa nyumbani. Watoto wanalazimika kuwa na adabu. Wakati wa kupiga video ya habari, kimya kinatawala. Bila shaka ubora wa kazi unaathirika kwa sababu hatuko katika mazingira tuliyozoea.”

Tayari Kanyinda ameandika kitabu kusimulia yale aliyopitia wakati akiugua Corona mwezi uliopita sababu ikiwa ni kwamba, “naona watu wanaonizunguka hawaamini kuhusu virusi vya Corona. Katika ushuhuda wangu najaribu kuelimisha wananchi wa DRC kuwa tubadili tabia. Hili janga watu bado hawaamini. Kiukweli Corona ipo DRC.”

Wizara ya afya ya DRC kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wengine, wanaendelea kuwekeza katika kujenga uwezo wa wafanyakazi wa ustawi wa jamii na wanasaikolojia ili waweze kusaidia watoto na familia kama ya Kanyinda ili ziweze kukabiliana na athari za muda mfupi na mrefu za virusi vya Corona.