Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukijitolea zaidi kupambana na corona, matokeo yanaweza kuwa mazuri-WHO

Nesi wa chumba cha dharura wakiwa wamejikinga pua na midomo katika Hospitali mjini Shenzhen nchini China
Man Yi
Nesi wa chumba cha dharura wakiwa wamejikinga pua na midomo katika Hospitali mjini Shenzhen nchini China

Tukijitolea zaidi kupambana na corona, matokeo yanaweza kuwa mazuri-WHO

Afya

Mkurugenzi Mkuu  wa shirika la afya duniani WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus hii leo akihutubia mkutano wa 146 wa bodi kuu ya shirika hilo mjini Geneva Uswisi ameeleza hatua iliyofikiwa hivi sasa kuhusu hali ya ugonjwa wa virusi vya corona.

Ameueleza mkutano huo kuwa kufikia muda huo alipokuwa akihutubia kuna jumla ya visa 17,238 ambavyo vimeshathibitishwa nchini China, huku vifo vikiwa vimefikia 361.

Dkt Tedros amenukuliwa akisema, “nje ya China, kuna visa 151 ambavyo vimethibitishwa katika nchi 23, kifo kimoja ambacho kimeripotiwa jana nchini Ufilipino.” 

Aidha ameueleza mkutano huo kuwa aliridhishwa na maelezo ya rais wa China Xi Jinping walipokutana nchini China ambapo rais huyo aliahidi kwa dhati kuwa wako tayari kuchukua hatua kwenye chanzo ili kuwalinda watu na pia kuzuia kusambaa kwa virusi katika nchi nyingine. “tuna mamlaka ya kufanya hivyo na hivyo ndivyo tutakavyofanya.” Rais Xi Jinping alimthibitishia Dkt Tedros.

“Kwa hivyo mlipuko huu unaweza kudhibitiwa, msifanye makosa, hali inakuwa mbaya zaidi. Lakini tukijitolea kwa kiwango chetu cha hali ya juu, matokeo yanaweza kuwa bora hata zaidi.” Amesisitiza Dkt Tedros.

Vilevile amkembushia kuwa isingekuwa ni juhudi za China, idadi ya visa nje ya China vingekuwa vingi zaidi na bado vinaweza kuwa lakini tuna fursa sasa kufanya kazi kwa bidii kuzuia hilo kutokea.