Skip to main content

Hakuna aliye na kinga dhidi ya COVID-19 Sudan Kusini, tupambane nayo pamoja:UNMISS 

Maafisa wa UNMISS wakizungumza na wenyeji katika soko lililoko mpakani
Video Screen Shot
Maafisa wa UNMISS wakizungumza na wenyeji katika soko lililoko mpakani

Hakuna aliye na kinga dhidi ya COVID-19 Sudan Kusini, tupambane nayo pamoja:UNMISS 

Afya

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umesema umedhamiria kulisaidia taifa hilo changa kabisa duniani kupambana na janga la corona au COVID-19 wakati huu likiwa katika harakati za kujikwamua kutoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenye.

Katika eneo la Abiemnhom Juba vijijini nchini Sudan Kusini hali ni bayana kwamba umasikini umeghubika eneo hili hasa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha maelfu kuzikimbia nyumba zao. Sasa janga jipya la corona linaloitikisa dunia linatoa tishio jipya kwa wakazi wa eneo hili.

Hivyo mpango wa Umoja wa Mataifa UNMISS ukiongozwa na mkuu wa mpango huo David Shearer umeamua kuchukua jukumu la kusaidiana na serikali kufanya kila liwezekanalo  kupambana na COVID-19 na kuwapunguzia madhila zaidi wananchi.

“Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika kila jimbo wameketi na kikosi kasi cha eneo hilo cha COVID-19 kuweka mikakati ya jinsi gani Umoja wa Mataifa utasaidia. Vikosi kazi hivyo vimeelezea kwamba hospitali nyingi na vituo viko katika hali mbaya hakuna umeme, maji, mapaa yanavuja, hakuna nafasi ya kutibu wagonjwa na hakuna vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya.”

Kwa kutambua hilo bwana Shearer amesema Umoja wa mataifa umeanza mradi mkubwa wa kutatua changamoto hizo ikiwemo kukarabati hospitali, kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa kwa kuwapa mahema 100, kurejesha huduma ya maji na kuweka vituo vya kunawa mikono lakini pia kutoa vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya.

“Hizi ni baadhi ya kazi ambazo zitaleta mabadiliko makubwa katika vita dhidi ya COVID-19, nasema tumedhamiria kufanya kila liwezekanalo kusaidia juhudi za serikali. Tuko pamoja katika janga hili iwe tunafanyakazi Umoja wa Mataifa au wanajamii, hakuna aliye na kinga dhidi ya COVID-19 , yeyote kati yetu anaweza kupata virusi bila kujali utaifa, kabila, imani au kazi gani tunayofanya. Hivyo tusiwasonte vidole wanaougua badala yake tushikamane na kuzingatia hatua za kuzuia ugonjwa huu ili tujilinde na kuwalinda wengine."

Hadi kufikia mwishoni mwa wiki Sudan Kusini iliorodhesha wagonjwa 120 waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona.