Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yasambaza tenki za maji sokoni kudhibiti COVID-19 Juba Sudan Kusini

Wagonjwa wa COVID-19 wamethibitika katika Kituo cha ulinzi wa raia cha UN mjini Juba Sudan Kusini
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Wagonjwa wa COVID-19 wamethibitika katika Kituo cha ulinzi wa raia cha UN mjini Juba Sudan Kusini

UNMISS yasambaza tenki za maji sokoni kudhibiti COVID-19 Juba Sudan Kusini

Afya

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS, katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona au COVID-19, wamesambaza tenki za maji katika maeneo ya soko yenye msongamano wa watu mjini Juba. 

Magari ya Umoja wa Mataifa yanashusha tenki za maji na wakati huo huo walinda amani wa UNIMISS wanapanga tofali katika soko mjini Juba Sudan Kusini,, mahali ambapo tenki hizo za maji zitawekwa.

Awali, kupitia katika kipindi cha redio, Afisa Mkuu wa Ofisi ya UNMISS inayoshughulikia masuala ya nje katika mji wa Juba na Yei, Geetha Pious ameeleza kuwa vituo vya maji vyenye tenki za ujazo wa  lita 3000 vitawekwa na wahandisi wa Bangladeshi, na walinda amani watakuwa wanakuja mara kwa mara kujaza maji. Pia watatumia wasaa huo kuelimisha watu kuhusu ugonjwa wa COVID-19.


Walinda amani raia wa Bangladesh kutoka katika kampuni mbili za uhandisi, kwa siku tatu wanashirikiana katika kuweka tanki hizi za maji katika maeneo yaliyopangwa. Meja Badrul anasema, “tuko hapa kwa niaba ya UNMISS tukiweka vituo vya maji. Hivi vituo vya maji ni kwa ajili ya wananchi wa Sudan Kusini kunawa mikono. Sisi kama kampuni ya uhandisi ya Bangladesh, mara zote tutasimama na watu.”
 
Tenki za maji tayari zimewekwa katika maeneo, na sasa magari yanayoongozwa na walinda amani yanaonekana yakileta maji na kuyajaza katika tenki. Jamii za wenyeji zinashukuru kwa juhudi za kukuza uelewa zilizofanywa na kikosi kazi cha ngazi za juu kuhusu COVID-19 na pia UNMISS. David ni kiongozi wa jamii katika eneo la Minuki anasema, “hatua hii ya kinga ni kitu ambacho kimetoka katika kikosi kazi cha ngazi ya juu. Virusi vya corona ni ugonjwa unaoambukiza sana ambao unaweza kuathiri jamii. Kwa hivyo ambacho UNMISS inaifanyia jamii kinathaminiwa sana.Ninafurahi sana na ninatumai kutakuwa na msaada zaidi.”
 
Kwa sasa, Sudan Kusini ina wagonjwa 194 wa COVID-19 waliothibitishwa, wawili kati yao wakiwawamethibitishwa katika vituo vya ulinzi wa raia na bila shaka juhudi hizo za UNMISS zitasaidia kuidhibiti hali.