Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imedhihirisha umuhimu wa ICT duniani:Guterres

Wasichana walioshiriki kwenye kongamano la kimataifa la wasichana na Habari, Mawasiliano na Teknolojia, ICT  huko Addis Ababa, Ethiopia tarehe 25 Aprili 2019
ITU/M.Tewelde
Wasichana walioshiriki kwenye kongamano la kimataifa la wasichana na Habari, Mawasiliano na Teknolojia, ICT huko Addis Ababa, Ethiopia tarehe 25 Aprili 2019

COVID-19 imedhihirisha umuhimu wa ICT duniani:Guterres

Utamaduni na Elimu

Janga la mlipuko wa virusi vya Corona au COVID -19 limedhihirisha umuhimu wa teknolojia ya Habari na mawasiliano TEHAMA au ICT kwa wasichana na dunia nzima umesema Umoja wa Mataifa.

 

Janga la mlipuko wa virusi vya Corona au COVID -19 limedhihirisha umuhimu wa teknolojia ya Habari na mawasiliano TEHAMA au ICT kwa wasichana na dunia nzima umesema Umoja wa Mataifa.

Kupitia ujumbe wake kuhusu siku ya wasichana katika ICT,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema siku hii ambayo lengo lake ni kuwachagiza wasichana kuingia katika taaluma ya tekinolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA) pia ni ya kuzitaka serikali , makampuni na wanazuoni kuunda mikakati ya kuwawezesha na kuwasaidia wasichana ambao wanataka kuingia katika taaluma hiyo ambayo imedhihirisha umuhimu wake zaidi wakati huu wa janga la COVID-19.

Bwana Guterres amesema “Wakati huu ambapo mabilioni ya watu wamesalia majumbani , biashara zimefungwa kuanzia New York hadi Nairobi, huku wahudumu wa afya wakilemewa kupita kiasi, mitandao ya kidijitali imekuwa na jukumu muhimu la kuifanya dunia kuendelea kufanyakaz. Inatufanya tuendelee kuungana, kusaidia wahudumu wa afya kuendelea kuwahudumia wagonjwa na kuwezesha watafiti ambao wanashirikiana kuweza kutengeneza chanjo.”

Akiunga mkono hoja hiyo katibu mkuu wa Muungano wa kimataifa wa mawasiliano ITU, Houlin Zhao amesema

“Katika msukusuko huu siku ya wasichana katika ICT ni muale wa matumaini, ni matumaini ya wanawake na wasichana hawa kote duniani ambao wanaona ahadi ya mustakbali bora katika teknolojia, sio tu kwa ajili yao peke yao bali kwa watu wote na jamii zinazowazunguka. Hakuna virusi hata viwe na nguvu kiasi gani vinaweza kupoteza matumaini hayo.”

Guterres amesisitiza kuwa teknolojia ya kidijitali itakuwa ndio ufunguo wa mafanikio kwani pia inazisaitda timu za watafiti kuelewa virusi hivi, tabia zake na jinsi ya kudhibiti kuenea kwake.

Hata hivyo amesema “Lakini wanawake wanapotengwa katika kazi hizo tunatoa nakala na kuongeza pengo la usawa wa kijinsia, tunaunda bidhaa ambazo hazizingatii mahitaji ya nusu ya watu na tunazidisha pengo la kijinsia la kidijitali”

Katibu Mkuu akaenda mbali zaidi akisisitiza “Kwa wanawake na wasichana wa leo nasema suluhu za kidijitali zitakuwa kitovu cha kila changamoto itakayokabili kizazi chenu. Ulimwengu hauwezi kumudu kupoteza talanta zenu.”

Kisha Katibu Mkuu akawaachia swali wasichana hawa akihoji “Taaluma gani za kazi zinaweza kuwa na tahamani zaidi ya kuwa mastadi wa ujuzi wa kidijitali ambao utasaidia kuokoa sayari yetu na watu wake”.?

Siku ya wasichana katika ICT huadhimishwa kila mwaka Aprili 23.