Janga la COVID-19 laongeza hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula duniani:EU/UN/USAID

21 Aprili 2020

Ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na shirika la Marekani la msaada wa kimataifa USAID inaonyesha kwamba janga la mlipuko wa virusi vya corona au COVID-19 linaweka njia panda mustakbali wa chakula na lishe.

Ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na shirika la Marekani la msaada wa kimataifa USAID inaonyesha kwamba janga la mlipuko wa virusi vya corona au COVID-19 linaweka njia panda mustakbali wa chakula na lishe. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya pamoja ya kila mwaka kuhusu mgogoro wa chakula na lishe iliyotolewa na muungano wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanyakazi kushughulikia mzizi wa njaa na lishe, inasema COVID-19 inatoa tishio jipya katika uhakika wa chakula na lishe.

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, la kuhudumia watoto UNICEF, la chakula na kilimo FAO, EU, na USAID yamesema ripoti hiyo iliyopewa jina “Muungano wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa chakula” inaonyesha kwamba mwishoni mwa mwaka 2019 watu milioni 135 katika nchi 55 walikabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula.

Ethiopia ikikabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula 2019, huku viwango vya njaaa na utapiamlo vikiongezeka kwa kiwango cha kutisha
© FAO/IFAD/WFP/Michael Tewelde
Ethiopia ikikabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula 2019, huku viwango vya njaaa na utapiamlo vikiongezeka kwa kiwango cha kutisha

Na zaidi ya hapo “katika nchi 55 zenye mgogoro wa chakula zilizoangaziwa kwenye ripoti hii watoto milioni 75 walikuwa na matatizo ya kudumaa na milioni 17 waathirika la kupoteza uzito kutokana na utapiamlo kwa mwaka 2019.”

Ripoti hiyo inasema hiki ni kiwango cha juu sana cha kutokuwa na uhakika wa chakula na utapiamlo kilichoorodheshwa na mtandao huo tangu kutolewa kwa ripoti ya kwanza mwaka 2017.

Mwaka huohuo wa 2019 ripoti imewaweka watu milioni 183 katika daraja la pili la kutokuwa na uhakika wa chakula ambalo ni sawa na kukabiliwa na njaa kubwa na kuwa katika hatihati ya kutumbukia katika mgogoro wa chakula endapo watakabiliwa na zahma nyingine kubwa kama janga la COVID-19.

Zaidi ya nusu ya watu hao milioni 135 walioangaziwa katika ripoti hii wanaishi barani Afrika, milioni 43 Mashariki ya Kati na Asia, na milioni 18.5 Amerika ya Kusini na Caribbea.

Nchi 10 zilizoathirika vibaya a uhakika wa chakula mwaka 2019 ni pamoja na Yemen, Congo DRC, Afghanistan, Venezuela, Bolivia, Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, Nigeria na Haiti.

Kichocheo kikubwa cha hali hii ripoti inasema ni Pamoja na vita ambavyo vimewasukuma watu milioni 77 kwenye hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula, mabadiliko ya tabia nchi yaliyowaathiri watu milioni 34 na kuyumba kwa uchumi ambayo kumewaacha watu milioni 24 bila uhakika wa chakula.

 Ripoti imependekeza kuchukuliwa hatua madhubuti hivi sasa ili kuwaepusha watu milioni 265 kutoka katika nchi za kipato cha chini kutumbukia katika janga kubwa zaidi la kutokuwa na uhakika wa chakula na baa la njaa.

Ukweli ni kwamba muda unatutupa mkono

David Beasley,mkuu wa mpango wa chakula duniani, akizuru Sanaa, Yemen amabko mgorgoro mkubwa wa njaa umekuwa ukiendelea kwa mwaka sasa.
WFP/Marco Frattini
David Beasley,mkuu wa mpango wa chakula duniani, akizuru Sanaa, Yemen amabko mgorgoro mkubwa wa njaa umekuwa ukiendelea kwa mwaka sasa.

Na katika kikao maalum cha baraza la Usalama kilichofanyika leo kwa njia ya mtandao kutathimini migogoro na uhakika wa chakula mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP David Beasely amesema “Dunia sio tu kwamba inakabiliwa na janga la kimataifa la afya lakini pia janga la kimataifa la kibinadamu.”

Ameongeza kuwa “ukweli ni kwamba muda unatutupa mkono hivyo hebu na tuchukue hatua kwa busara na kwa haraka. Ni muhimu sana kuja Pamoja kama jumuiya ya kimataifa kupambana na janga hili la COVID-19” 
Amesema janga hilo limesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu tangu vita vya pili vya dunia hasa ukizingatia kwamba dunia tayari inakabiliwa na dhoruba kubwa kuanzia mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili, vita , njaa na mengineyo.

Ombi la Msaada

WFP imeliomba Bsaraza la Usalama kuongoza njia katika juhudi za kimataifa kupambana na COVID-19. 
Mosi na kipaumbele cha kwanza amaesema tunahitaji amani, amewataka wote wanaohusika katika mapigano kuruhusu na kutoa fursa kwa wahudumu wa misaada ya kibinadamu kuzifikia jamii zisizojiweza na kuratibu msaada wa kuokoa Maisha Pamoja na dola milioni 350 za ufadhili mpya ili kuweka mtandao wa kiufunzi kuhakikisha mnyororo wa kimataifa wa usambazaji msada unaendelea.

Bwana Beasley pia ameelezea haja ya kuwa na mfumo wa tahadhari ya mapema “Endapo hatotojiandaa na kuchukua hatua sasa  kupata fursa ili kuepuka pengo la ufadhili  na usumbufu katika biashara huenda tukakabiliwa na baa la njaa kama lililoelezwa kwenye biblia katika miezi michache ijayo.”

Uhusiano baina ya migogoro na uhakika wa chakula

Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu
©FAO/Giuseppe Carotenuto
Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu

Mkurugenzzi mkuu wa shirika la FAO Qu Dongyu jinsi gani ripoti ya kimataifa ya mgogoro wa chakula ya 2020 ina uhusiano na migogoro na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

Amesema “hatua za pamoja zinahitajika miongoni mwa wadau wa masuala ya kibinadamu, maendeleo na amani kushughulikia mizizi ya tatizo sugu la kutokuwepo kwa uhakika wa chakula.”
Amesema utabiri wa uhakika wa chakula 2020 si mzuri na hivyo ni muhimu kuwa na tahadhari ya mapema na kuchukua hatua haraka kuzuia kutokuwa na uhakika wa chakula kunakosababishwa na migogoro.
Licha vita, majanga ya asili, mdororo wa kiuchumi na sasa COVID-19 vinavyowasukuma watu kutumbukia katika hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula  Bwana. Qu ana matumaini kwamba “Kwa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mabadiliko haya tunaweza kuchukua hatua mapema na kupunguza athari zake.”
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter