UNICEF, Microsoft na Cambrigde watangaza Pasipoti ya kujifunza 

20 Aprili 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na Kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Microsoft hii leo mjini New York Marekani wametangaza upanuzi wa jukwaa la kimataifa la kujifunza kuwasaidia watoto na vijana ambao wameathiriwa na COVID-19 kuendelea na elimu yao wakiwa nyumbani.

Jukwaa hilo lililopewa jina ‘Pasipoti ya kujifunza’ lilianza kama ushirikiano kati ya UNICEF, Microsoft na Chuo Kikuu cha Cambridge pamoja na idara zake za Cambridge University Press inayohusika na uchapishaji wa vitabu na ile nyingine ya tathimini. Jukwaa hilo limeandaliwa kutoa elimu kwa watoto waliofurushwa na pia watoto wakimbizi kupitia mfumo wa dijitali. Hivi sasa jukwaa hilo imefanyiwa upanuzi mkubwa na wa haraka ili kusaidia ngazi za mitaala ya nchi kwa ajili ya watoto na vijana ambao shule zimelazimika kufungwa kutokana na COVID-19. Mfumo huo pia utatoa rasilimali kwa walimu na waelimishaji wengine. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema, “kutoka kufungwa kwa shule, kutengwa, hadi hali ya hofu na wasiwasi, athali za janga hili zinaathiri watoto duniani kote. Tunahitaji kuungana na kutafuta kila njia ya kuwafanya watoto waendelee kujifunza na kuwasaidia kupita katika kipindi hiki kigumu. Tukiwa na washirika wetu wa muda mrefu kama Microsoft tunaweza kupeleka haraka suluhisho la ubunifu. Marekebisho yaliyofanywa katika mfumo huu wa sasa wa Pasipoti   ya kujifunza ni ukumbusho mzuri wa kile tunachoweza kukifikia kwa pamoja kwa ajili ya watoto wakati janga linavyozidi ulimwenguni.”

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za UNESCO, wanafunzi bilioni 1.57 wameathiriwa na kufungwa kwa shule katika zaidi ya nchi 190 duniani kote. 

Pasipoti ya kujifunza ambayo imekuwa ikiendelezwa kwa miezi 18 iliyopita, ilikuwa ianze kwa programu ya majaribio katika mwaka huu wa 2020. Wakati janga hili la COVID-19 lilipotokea na shule zikafungwadunaini kote, programu hiyo ililazimika kufanyiwa upanuzi mkubwa wa haraka. Hivi sasa nchi zote mtaala ambao unaweza kufundishwa kupitia mtandaoni wataweza kupitisha masomo yao kwa watoto na vijana walio na vifaa vya kielektroniki majumbani.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter