Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi wa dunia kuporomoka vibaya mwaka huu wa 2020-IMF

IMF imetoa tolea la kuonesha hatua zinazochukuliwa na serikali kulina watu wake dhidi ya virusi vya corona na uchumi katika zama hizi.
IMF
IMF imetoa tolea la kuonesha hatua zinazochukuliwa na serikali kulina watu wake dhidi ya virusi vya corona na uchumi katika zama hizi.

Uchumi wa dunia kuporomoka vibaya mwaka huu wa 2020-IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Mtazamo mpya uliotolewa na shirika la fedha duniani IMF kuhusu mwenendo wa uchumi duniani kwa mwaka huu 2020 unaonyesha kuwa ukuaji wa uchumi utakuwa katika hali hasi ya asilimia -3% kwa sababu ya mlipuko wa janga la virusi vya Corona au COVID-19.

Akizungumzia mtazamo huo mjini Washington Marekani kwenye mikutano ya msimu wa chipukizi ya shirika hilo iliyoanza Jumanne mchumi mkuu wa IMF Gita Gopinath amesema,“Chini ya matarajio kwamba janga hili na mbinu za kulidhibiti zitafanikiwa katika robo ya pili yam waka huu katika nchi nyingi duniani na kisha kumalizika katika nusu ya pili yam waka, tunakadiria kwamba ukuaji wa uchumi duniani 2020 kushuka hadi asilimia hasi -3.”

Ameongeza kuwa hii ni chini ya makadirio ya asilimia 6.3 yaliyotolewa mwezi Januari, ni kiwango kikubwa katika muda mfupi na hali hii inakuwa ni hali mbaya zaidi tangu kipindi cha kuporomoka kwa uchumi wa dunia na mbaya zaidi kuliko mdororo wa uchumi wa 2008.

Gopinath amesema hata kama janga hili litadhibitiwa mwishoni mwa mwaka huu bado IMF inachokiona ni hali ndogo sana ya kujikwamua kwa mwaka 2021.“Kwa kukisia kwamba gonjwa hili litakwisha katika nusu ya pili yam waka 2020 na kwamba hatua na sera zilizochukuliwa ulimwenguni kote ni bora na zitazuia kufilisika kwa makampuni, upotevu wa ajira na uwezo wa mfumo wa kifedha, tunakadiria kwamba ukuaji wa uchumi mnamo 2021utarudi kwa asilimia 5.8, huu utakuwa ni ukuaji wa sehemu ndogo tu kwani kiwango cha shughuli za uchumi kinatarajiwa kusalia chini ya kiwango ambacho tulikuwa tunakitarajia kwa 2021 kabla ya mlipuko wa virusi.

IMF imeweka bayana kwamba kujikwamua kikamilifu kiuchumi kutakuja tu endapo janga hili la kiafya litakuwa limedhibitiwa kikamilifu. Na kwa mantiki hiyo imesisitiza umuhimu wa kupiga jeki mikakati ya kuinua uchumi wakati huu wa mgogoro na kutumai kwamba kiwango cha madeni kitashuka baada ya uchumi kutengamaa.