Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pato la kimataifa kushuka kwa asilimia 0.9 mwaka  2020 sababu ya COVID-19:DESA

Mji wa London, Uingereza
Unsplash/Ali Yaqub
Mji wa London, Uingereza

Pato la kimataifa kushuka kwa asilimia 0.9 mwaka  2020 sababu ya COVID-19:DESA

Ukuaji wa Kiuchumi

Uchumi wa dunia unaweza kushuka kwa asilimia 0.9 mwaka huu wa 2020 kutokana na janga la virusi vya Corona, COVID-19, na uzalishaji wa dunia utashuka hata zaidi endapo vikwazo vya kiuchumi vitaendelea katika robo ya tatu ya mwaka huu, na kama bajeti za kupambana na janga hili hazitosaidia kipato na wateja, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo Jumatano na Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na masuala ya kijamii DESA, imesisitiza kuwa kuongezeka kwa vikwazo vya watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na vikwazo vingine Ulaya na Marekani vinaathiri vibaya sekta za huduma hususan viwanda ambavyo vinahusiha watu kukutana kama vile maduka, masuala ya starehe, huduma za mahoteli na usafiri.

Ripoti hiyo imesema “Kwa pamoja sekta hizi zina zaidi ya robo ya ajira zote za kuchumi. Wakati biashara zikipoteza pato ukosefu wa ajira unatarajiwa kuongezeka na hivyo kuathiri usambazaji wa bidhaa na mahitaji pia hali ambayo inaathiri pakubwa uchumi”

Ukubwa wa athari

Ripoti hiyo ya DESA inasema kwa kutathimini ukubwa wa athari iwe ni mdororo wa wastani au mkubwa wa uchumi utategemeana na muda wa kuendelea kwa vikwazo hivyo kwa watu na shughuli za kiuchumi katika chumi zilizoendelea na kwa kiwango cha uchumi lakini pia utendaji wa bajeti zilizowekwa kukabiliana na mgogoro huu.

 

Ripoti inasema mkakati mzuri wa kichocheo cha fedha, kuweka kipaumbele katika matumizi ya kiafya ili kudhibiti maambukizi ya virusi na kutoa msaada wa kipato kwa ajili ya kaya zilizoathirika sana na COVID-19 kunaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa mdororo wa uchumi  wa kiwango kikubwa.

Mkuu wa DESA Liu Zhenmin akisisitiza hilo amesema “Hatua za haraka na madhubuti za kisiasa zinahitajika sio tu kwa ajili ya kudhibiti janga hili na kuokoa maisha, lakini pia kwa kulinda wale wasiojiweza katika jamii zetu kutokana na mdororo wa uchumi na kusaidia ukuaji wa uchumi na utulivu wa kifedha.”

Athari za kiuchimi zinasambaa dunia nzima

Athari za kiuchumi kutokana na vikwazo vya muda mrefu katika nchi zilizoendelea hivi karibuni zutahamia katika nchi zinazoendelea kupitia biashara na uwekezaji imesema ripoti.

Imeongeza kuwa kushuka kwa kiasi kikubwa kwa mtumizi ya walaji katika Muungano wa Ulaya na Marekani kutapunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nchi zinazoendelea. 

Shehena za usafirishaji mizigo kwenye bandari katika Jamhuri ya Kidmokrasia ya São Tomé na Príncipe
UNCTAD/Jan Hoffmann
Shehena za usafirishaji mizigo kwenye bandari katika Jamhuri ya Kidmokrasia ya São Tomé na Príncipe

Na zaidi ya hapo uzalishaji wa viwandani wa kimataifa unaweza kushuka kwa kiasi kikubwa ukizingatia uwezekano kuathirika kwa mnyororo wa kimataifa wa usambazaji

“Kwa kuangalia katika hali mbaya zaidi pado la kimataifa GDP limnaweza kushuka kwa asilimia 0.9% mwaka 2020 badala ya kuongezeka kwa asilimia 2.5%. Uzalishaji wa dunia unaweza kushuka Zaidi endapo vikwazo katika shughuli za kiuchumi  vitaendelea hadi robo ya tatu yam waka hu una endapo bajeti za kukabiliana na hali hiyo hazitosaidia kipato na watumiaji kununua bidhaa.” Imeonya ripoti hiyo.

Ikilinganisha na miaka iliyopita ripoti inasema wakati wa mdororo wa uchumi wa mwaka 2009 uchumi ulishuka kwa asilimia 1.7%.

Nchi zisisojiweza zinaathirika zaidi

Ripoti hiyo imesema nchi zinazoendelea hususani zile ambazo zinategemea sekta ya utalii na usafirishaji nje wa bidhaa zinakabiliwa na ongezeko la hatari za kiuchumi. 

Kusitishwa kwa ghafla kuwasili kwa watalii kutaathiri sekta ya utalii katika mataifa madogo ya visiwa vinavyoendelea (SIDS) sekta ambayo inaajiri mamilioni ya watu wenye ujuzi mdogo.

Na kuporomoka kwa kipato kitokanacho na bidhaa na kubadilika kwa uingiaji wa mitaji ni ishara ya ongezeko la madeni kwa wengi ambao uchumi wao unategemea bidhaa.

Ripoti imeweka bayana kwamba serikali huenda zikalazimika kupunguza matumizi ya umma katika wakati ambapo wanahitaji kuongeza matumizi ili kudhibiti kusambaa kwa mlipuko wa virusi na kusaidia matumizi na uwekezaji.

Mgogoro wa kiuchumi utakuwa na athari mbaya katika maendeleo endelevu. Na COVID-19 inaathiri kwa kiasi kikubwa Zaidi mamilioni ya wafanyakazi wenye ujira mdogo katika sekta za hudumaambao mara nyingi hawana ulinzi wa ajira zao na wanafanya kazi kwa karibu na wengine.

Bila kuwa na msaada wa kutosha wa kipato watu wengi watatumbukia katika umasikini hata katika nchi zilizoendelea na kusababisha kuongezeka kwa kiwango ambacho tayari kinashuhudia cha pengo la usawa. 

Pia imesema kuwa athari za kufungwa kwa shule kunaweza kusababisha mgawanyiko shuleni na uwezekano wa athari za muda mrefu.

Hali halisi

Ripoti imebaini kwamba hali ya mlipuko wa COVID-19 inazidi kuwa mbaya, athari za kiuchumi zinaongezeka, vikichangiwa na ukuaji mdogo wa uchumi na ongezeko la pengo la usawa.

Inasema hata katika nchi nyingi zenye uchumi mkubwa idadi kuwa ya watu wake hawana rasilimali fedha za kutosha kuishi juu ya kiwango cha kitaifa cha umasikini kwa miezi mitatu.

Mathalani kwa mataifa ya Italia na Hispania yaliyoathirika zaidi inakadiriwa kwamba asilimia 27 Italia na 40  Hispania ya watu hawana akiba ya kutosha kuwaweseha kutofanya kazi kwa Zaidi ya miezi mitatu.

“Ingawa tunahitaji kutoa kipaumbele kwa hatua za kiafya za kukabiliana na janga hili kwa gharama zozote zile , ni lazima tusisahau athari zake kwa watu wasiojiweza nah ii inamaanisha nini kwa maendeleo endelevu. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tuna mnepo wa kujikwamua kutoka kwenye janga hili na kurejea katika utumizaji wa malengo ya maendeleo endelevu.” Amesema Elliott Harris mchumi mkuu na msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

TAGS:COVID-19, DESA, coronavirus, uchumi, UN