Janga la COVID-19 halijamalizika , muwe makini katika matumizi yenu:IMF

Shirika la fedha duniani IMF limeziasa nchi na watu wote kuwa makini katika matumizi yao kwani athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la corona au COVID-19 hazijaisha na zitaendelea kwa muda.
Kwa mujibu wa shirika hilo mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na COVID-19 utaacha majeraha ya muda mrefu katika maisha ya watu kuanzia kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na kufungwa kwa shule, kushuka kwa thamani ya fedha kutokana na watu na makampuni kufilisika na changamoto kubwa katika sera za siku zijazo kutokana na nchi kuwa na mzigo mkubwa wa madeni huku makundi ya waliokuwa hatarini na masikini sasa kutumbukia katika ufukara zaidi.
Taarifa ya IMF iliyotolewa Jumatatu imesema hatua zilizochukuliwa na watunga sera ikiwemo kutoka nchi 20 zilizo na uchumi mkubwa duniani au G20 zimesaidia kwa kiasi fulani kuepusha zahma kubwa zaidi ya kiuchumi kutokana na COVID-19, kwa kutoa dola trilioni 11 za msaada wa lazima kwa watu binafsi, makampuni ya biashara na sekta za huduma za afya tangu kuzuka kwa janga hilo.
Hata hivyo taarifa hiyo imeonya kwamba asilimia kubwa ya msaada huo sasa taratibu unapungua na faida kama mgao wa fedha kwa kaya, au kusitisha malipo ya kodi au mikopo ya dharura kwa wafanyabiashara vimekwisha au vitamalizika mwisho wa mwaka huu wakati ambao kiwango cha ukosegfu wa ajira kutokana na athari za COVID-19 bado kikitarajiwa kuwa cha juu.
Kwa mantiki hiyo IMF imependekeza ,mosi msaada uendelee kwa wakati wote wa janga la COVID-19 kwani kuukatisha mapema utasababisha zahma zaidi katika maisha ya watu, na kuongeza kufilisika kwa makampuni na biashara hali ambayo itaathiri juhudi za kujikwamua na janga hili.
Na pili shirika hilo limesema baada ya janga hili sera lazima ziende sanjari na hali halisi na kujenga mnepo kwani safari itakuwa ngumu na itachukua muda hivyo huu ni wakati wa kumakinika katika matumizi na kushirikiana kujenga mustakbali bora.