Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikakati ya kudhibiti COVID-19 inatofautiana; WHO yatoa mwongozo wa kufuata

Wanakijiji nchini Sudan Kusini wakijifunza kuhusu hatari ya viusi vya Corona. Mafunzo haya yanatolewa na shirika mdau na UNICEF.
© UNICEF/Brian Ongoro
Wanakijiji nchini Sudan Kusini wakijifunza kuhusu hatari ya viusi vya Corona. Mafunzo haya yanatolewa na shirika mdau na UNICEF.

Mikakati ya kudhibiti COVID-19 inatofautiana; WHO yatoa mwongozo wa kufuata

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, kesho litachapisha mwongozo wenye taarifa zaid za kuwezesha nchi kuchukua hatua za kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 sambamba na kuwa msingi wa kuamua iwapo kurejesha shughuli za kiuchumi na kijamii au la.
 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi.

Dkt. Tedros amesema hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba mataifa mbalimbali katika kukabiliana na COVID-19, yamechukua hatua nyingine zinazohatarisha haki za binadamu, na nyingine hata kusababisha watu kushindwa kujipatia kipato.
“Unaishi vipi kwenye marufuku ya kutoka nje ilhali unategemea kibarua ili uweze kupata chakula? Ripoti mpya kutoka maeneo mbalimbali dunia zinaelezea jinsi gani watu wako hatarini kusalia bila chakula,” amesema Dkt. Tedros.

Amesema, shule nazo zimefungwa ambapo watoto bilioni 1.4 hawako shuleni hali ambayo amesema imesitisha mafunzo yao, huku ikifungua milango ya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto huku wengine wakikosa mlo ambao walizoea kupata shuleni.

Nchi zilizoendelea kama Marekani, watoto wanaendelea na masomo kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona
© UNICEF/Lisa Adelson
Nchi zilizoendelea kama Marekani, watoto wanaendelea na masomo kwa njia ya mtandao wakiwa nyumbani katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona

Dkt.Tedros amesema kwamba suala la kuzuia watu kuchangamana ni moja tu ya mikakati lakini kila serikali inapaswa kutathmini mazingira yake, huku ikilinda raia wake hususan wale walioko hatarini zaidi.

Ni kwa mantiki hiyo amesema mkakati huo mpya unaweka kwa muhtasari kile ambacho wamejifunza na kubainisha hatua za kuchukua ambapo kuna vipengele sita ambavyo nchi zinapaswa kuzingatia pindi zinapotaka kuondoa vikwazo au marufuku zilizowekwa katika kudhibiti COVID-19.

Vipengele 6 pendekezwa

Mosi ni kuhakikisha kuwa maambukizi yanadhibitiwa, pili, mfumo ya afya iliyopo ina uwezo wa kutambua, kuchunguza, kutenga na kutibu kila mgonjwa na mwambata wake na tatu, Hatari za mlipuko zinapunguzwa hasa kwenye maeneo ya hospitali, vituo vya afya na makazi ya kuuguza.

Kipengele cha nne, mikakati ya kinga iwepo maeneo ya makazini, shuleni na kwingineko ambako ni lazima watu waende na tano, kuwepo na hatua za kudhibiti maambukizi yanayoletwa na hatimaye sita, jamii zielimishwe vya kutosha na ziwezeshwe kuendana na mazingira mapya yaliyojitokeza.

WHO imesisitiza kuwa kila nchi inapaswa kutekeleza mikakati ya kina ya kupunguza maambukizi na kuokoa maisha, kwa lengo la kuwa na kiwango cha chini cha maambukizi na hatimaye kutokomeza kabisa maambukizi.

Hata hivyo Dkt. Tedros amekumbusha kuwa ni lazima kuwepo na mizani katika kutibu COVID-19 na magonjwa mengine wakati huu ambapo mifumo ya afya imezidiwa sambamba na kushamiri kwa athari za kiuchumi na kijamii.

Dkt. Tedros ametumia hotuba yake ya leo pia kushuruku Uingereza kwa mchango wake wa zaidi ya dola milioni 218 katika harakati za kimataifa za kutokomeza COVID-19.
.