Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumeanza rasmi chanjo ya majaribio ya dhidi ya COVID-19: WHO

Mtu akipatiwa chanjo (Maktaba)
PAHO.WHO.Jane Dempster
Mtu akipatiwa chanjo (Maktaba)

Tumeanza rasmi chanjo ya majaribio ya dhidi ya COVID-19: WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO leo limesema siku 60 baada ya sampuli za virusi vya Corona au COVID-19 kuwasilishwa kwa shirika hilo na Cina,  chanjo ya kwanza ya majaribio imeanza.

Akizungumza katika mkutano wa kila siku na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema “haya ni mafanikio makubwa, tunawapongeza watafiti kote duniani ambao wamekuja pamoja ili kutathimini majaribio ya tiba. Majaribio madogomadogo ya njia mbalimbali yanaweza yasitupe ushahidi wa kutosha , tunahitaji tiba yoyote ambayo itatusaidia kuokoa maisha.”

Ameongeza kuwa WHO na washirika wake wanaandaa utafiti katika nchi nyingi ambako baadhi ya nchi hizo dawa hizi ambazo hazijajaribiwa zitalinganishwa .

Amesema utafiti huo mkubwa unaandaliwa ili kukusanya takwimu zinazohitajika kuonyesha matibabu yapi yanafayakazi zaidi.

Utafiti huo Dkt. Tedros amesema umepewa jina la “Majaribio ya mshikamano”.

Mshikamano huu wa majaribio unatoa muongozo ambao unataziwezesha hospitali ambazo zimezidiwa kushiriki.

Mkurugenzi huyo mkuu amesema tayari nchi kadhaa zimethibitisha kwamba zitashiriki utafiti huo wa  Mshikamano wa majaribio zikiwemo Argentina, Bahrain, Canada, Ufaransa, Iran, Norway, Afrika Kusini, Hispania, Uswisi na Thailand na amesema anaamini nchi nyingine nyingi zitajiunga.

Naendelea kutiwa moyo na jinsi nchi nyingi zinavyoonyesha mshikamano kote duniani “ amesema Dkt. Tedros na kuongeza kwamba mfuko  wa hatua za mshikamano dhidi ya COVID-19 hadi sasa umeshakusanya zaidi ya dola milioni 43 kutoka kwa watu zaidi ya 173,000 na mashirika ikiwa ni siku chache tu tangu ulipozinduliwa.

Ninapenda kuishukuru hususan FIFA kwa mchango wake wa dola milioni 10, juhudi hizi na zingine zinanipa matumaini kwamba kwa pamoja tunaweza na tutashinda."  amesema Dkt. Tedros.

Amesisitiza kwamba virusi hivi ni tishio kubwa lakini pia ni fursa ya kuja pamoja kukabiliana na adui huyu mkubwa dhidi ya ubinadamu.