Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka kupanga safari za ndege hadi kusambaza vifurushi vya mlo; UNWTO yachukua hatua

Wakala wa safari amelazimika kubadili biashara yake ili aweze kuhusika kwenye kusambaza vyakula kwa familia zilizoathirika na virusi vya Corona
Wang Xiang
Wakala wa safari amelazimika kubadili biashara yake ili aweze kuhusika kwenye kusambaza vyakula kwa familia zilizoathirika na virusi vya Corona

Kutoka kupanga safari za ndege hadi kusambaza vifurushi vya mlo; UNWTO yachukua hatua

Afya

Shirika la utalii la Umoja wa mataifa, UNWTO, limetoa mapendekezo ya kusaidia sekta ya utalii wakati huu ambapo ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 umetikisa sekta hiyo kote ulimwenguni.
 

Mapendekezo hayo ni sehemu ya kwanza ya matokeo ya vikao ya kamati ya kimataifa ya utalii iliyoundwa kushughulkia janga la sasa, ikijumuisha wawakilishi kutoka sekta ya utalii duniani pamoja na Umoja wa Mataifa. 

Taarifa ya UNWTO iliyochapishwa katika wavuti wake inasema kuwa “Kwa kutambua kuwa sekta ya utalii ni moja ya sekta zilizoathiriwa zaidi duniani kutokana na janga la Corona, mapendekezo yanalenga kusaidia serikali , sekta ya binasi na jamii ya kimataifa kukabiliana na dharura isiyo ya kawaida ya kijamii na kiuchumi ambayo ni COVID-19.”

Mapendekezo hayo yako 23 lakini yamegawanywa katika sehemu kuu 3 ambazo ni;

1.  Kushughulikia janga huku athari zikipunguzwa

Mapendekezo muhimu yanataka watu waendelee kutunza ajira zao, kusaidia waliojiajiri, kuhakikisha kuna fedha au ukwasi, kupitia upya kodi, husiana na kutunza kazi, kusaidia wafanyikazi waliojiajiri, kuhakikisha ukwasi, kukuza ustadi wa ujuzi na kufanya mapitio ya kodi, gharama na kanuni zinazohusiana na utalii.  Mapendekezo haya yamezingatia hali ya sasa ya mdororo wa kiuchumi.

2. Kutenga mafungu ya fedha ili kuchochea ukwamukaji

Seti hii ya Mapendekezo inasisitiza umuhimu wa kutoa kichocheo cha kifedha, pamoja na sera nzuri za ushuru, kuondoa vizuizi vya kusafiri mara tu dharura ya kiafya inaporuhusu, kukuza uhamasishaji wa visa, kukuza uuzaji na ujasiri wa watumiaji, ili kuharakisha kuimarika. Mapendekezo hayo pia yanataka utalii uwekwe katikati ya sera za kitaifa za kuimarisha na mipango.

3. Kujiandaa kwa ajili ya kesho

Kusisitiza uwezo wa kipekee wa utalii wa kuongoza ukuaji wa ndani na kitaifa na kimataifa ambapo mapendekezo yanataka msisitizo mkubwa kuwekwa kwenye mchango wa sekta hiyo kwenye ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kujenga mnepo kutokana na mafunzo yaliyopatikana na janga la sasa. Mapendekezo hayo yanataka serikali na watendaji wa sekta binafsi kuwa mipango ya utayari, na kutumia fursa hii kugeukia uchumi wa mzunguko.

Akizungumzia mapendekezo hayo, Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili amesema , “mapendekezo haya mahususi yanapatia nchi orodha ya hatua zinazoweza kuchukuliwa kusaidia sekta yetu kuendeleza kazi na kusaidia kampuni zilizo hatarini kwa wakati huu. Kuzuia athari za ajira na ukwasi, kulinda walio hatarini zaidi na kujiandaa kukwamuka tena, mambo haya yote lazima yawe vipaumbele vyetu muhimu.” 

Hata hivyo nyaraka yenye mapendekeo hayo  itakuwa ikifanyiwa marekebisho kila wakati kuligana na mwelekeo wa janga la Corona na ukweli na uhalisia katika kila nchi.