Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Virusi vya Corona na utalii; UNTWO yapaza sauti

Watu wakiwa wamevaa barakoa kujikinga na virusi vya Corona. Hapa ni uwanja wa  ndege wa kimataifa wa Narita jijini Tokyo, Japan
UN News/Li Zhang
Watu wakiwa wamevaa barakoa kujikinga na virusi vya Corona. Hapa ni uwanja wa ndege wa kimataifa wa Narita jijini Tokyo, Japan

Virusi vya Corona na utalii; UNTWO yapaza sauti

Afya

Wakati virusi vya Corona, COVID-19 vikiendelea kuibua sintofahamu duniani hivi sasa, shirika la utalii la Umoja wa Mataiaf, UNWTO limesema linashirikiana na shirika la afya ulimwenguni, WHO na wadau wengine kusaidia mataifa kutekeleza mikakati ya kupunguza rabsha zisizo za lazima katika safari na biashara za kimataifa.

Taarifa  ya UNWTO  iliyotolewa leo mjini Madrid nchini  Hispania imesema kuwa, “sekta ya utalii imejizatiti kuweka mbele afya ya binadamu. Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kuhakikisha kuwa tunaweza kuchangia vyema katika kudhibiti virusi hivi vya Corona.”

Kwa mantiki hiyo taarifa hiyo imesema kuwa UNWTO na WHO wanashirikiana kwa karibu na wadau wengine kuhakikisha serikali zinaweka mikakati ya kiafya.

Shirika hilo limesema kuwa hatua za sekta ya  utalii zinapaswa kuwa za kuaminika na kuwiana na tishio la afya ya umma na kwa kuzingatia tathmini iliyofanyika katika nchi husika kwa kushirikiana na kila mdau kwenye sekta hiyo kwa mujibu wa mwongozo na mapendekezo ya WHO.

“UNWTO na WHO ziko tayari kushirikiana kwa karibu na jamii nan chi ambazo tayari zimeathiriwa na virusi vya Corona ili kujenga mustakabali wenye mnepo zaidi kwa jamii. Vizuizi vya safari vinavyokwenda kinyume cha hali ya sasa  vinaweza kusababisha rabsha kwenye safari za kimataifa, ikiwemo madhara kwenye sekta ya utalii,”  imesema taarifa hiyo.

Tarehe 30 mwezi uliopita wa Januari, Mkurugenzi  Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Gebreyesus alitangaza kuwa mlipuko wa COVID-19 ni dharura ya afya ya umma duniani na inatia hofu na hivyo kutangaza mapengekezo ya muda.

Hata hivyo WHO haikupendekeza vizuizi vya safari au vya biashara kwa kuzingatia taarifa zilizopo hivi sasa.

WHO inashirikiana na wataalamu duniani, serikali na wadau wengine kupanua wigo wa ufahamu wa kisayanasi wa virusi hivyo vipya, kufuatilia ueneaji wake na kutoa ushauri kwa nchi.